Albanese: Vikwazo dhidi yangu si lolote kulinganisha na masaibu wanayopitia Wapalestina
-
Francesca Albanese
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina amepuuzilia mbali vikwazo vilivyowekwa hivi karibuni na Marekani kutokana na msimamo wake wa kuukosoa utawala wa Israel, akisema kuwa vikwazo hivyo si lolote si chochte ikilinganisha na masaibu wanayoyastahamili na kupitia raia wa Palestina katika ardhi yao.
Francesca Albanese amehojiwa na televisheni ya Press ya nchini Iran na kutaja sababu zilizomfanya kusonga mbele ya kazi yake licha ya kuandamwa na hujuma za kisiasa zinazoongozwa na Marekani katika miezi ya karibuni kutokana na uungaji mkono wake mkubwa kwa haki za Wapalestina.
"Nimekuwa nikishambuliwa kama mtu yeyote anayesema ukweli, lakini hii si lolote ikilinganishwa na yale yanayowapata Wapalestina kwa sasa.
Albanese amesema ni jambo lisilokubalika kuwekewa vikwazo kwa sababu ni kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Hati ya umoja huo kuhusu kinga. Amesema vikwazo dhidi yake vinapaswa kuondolewa.
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina amesema: Anatarajia umoja huo utachukua hatua na kushughulikia suala hilo kidiplomasa na kisiasa na Marekani ili kuhakikisha kuwa suala hili linapatiwa ufumbuzi kwa sababu halikubaliki.
Bi Francesca Albanese ambaye ni msomi Muitaliano katika taaluma ya sheria na mtetezi wa haki za binadamu anayeheshimika kimataifa, amekuwa akifichua mara kwa mara jinai za kimfumo za Israel dhidi ya Wapalestina.

Mwezi uliopita, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilimwekea vikwazo Albanese ikimlaumu kwa kuichochea Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita Yoav Gallant kutokana na mauaji ya kimbari na jinai za kivita dhidi ya Wapalestina.
Marekani imechukua hatua hii kama sehemu ya juhudi za kuwaadhibu wale wote wanaokosoa vita na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.