Askari waliostaafu Marekani watishia kuwachinja Waislamu Texas
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12937-askari_waliostaafu_marekani_watishia_kuwachinja_waislamu_texas
Wanajeshi waliostaafu katika jimbo la Texas nchini Marekani wametishia kuwakata vichwa kwa mapanga Waislamu watakaoenda kutekeleza ibada ya swala katika msikiti mmoja jimboni hapo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 09, 2016 09:17 UTC
  • Askari waliostaafu Marekani watishia kuwachinja Waislamu Texas

Wanajeshi waliostaafu katika jimbo la Texas nchini Marekani wametishia kuwakata vichwa kwa mapanga Waislamu watakaoenda kutekeleza ibada ya swala katika msikiti mmoja jimboni hapo.

Sajenti Jason Babcock, ofisa wa polisi wa mji wa Wataunga amesema kuwa, wanashirikiana na Polisi ya Upelelezi Marekani FBI kuchunguza sauti ya askari mkongwe wa Marekani katika jimbo la Texas aliyetuma ujumbe wa sauti kwa waumini wa Kiislamu katika mji huo akiwaonya dhidi ya kwenda kuswali katika Msikiti wa Al-Sahaabah.

Kuenea kwa chuki na hofu dhidi ya Uislamu Marekani

Katika ujumbe huo wa sauti, askari huyo aliyestaafu amesema kuwa maveterani wengine wa kijeshi wa Marekani katika jimbo la Texas wako tayari kumchinja Muislamu yoyote atayeenda katika msikiti huo.

Alia Salem, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la Marekani katika eneo la Dallas sambamba na kulaani kitendo hicho, amesema baraza hilo limekuwa likipokea malalamiko kutoka kwa wasimamizi wa msikiti huo ambao wamekuwa wakitishiwa maisha kwa njia ya simu na watu wasiojulikana.

Maandamano ya Waislamu Marekani kulaani uenezaji wa chuki dhidi ya Uislamu

Julai 24, mamia ya Waislamu nchini Marekani waliandamana kupinga hatua za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika mji wa Washington DC huku wakipiga nara kulaani uenezaji wa vitendo vya chuki dhidi yao.

Ripoti ya mwezi Juni mwaka huu ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Berkeley jimboni California ilifichua kuwa, mashirika yapatayo 74 yametoa kiasi cha dola milioni 206 za Marekani kwa ajili ya kutumika kueneza chuki na hofu dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.