Dunia yalaani mashambulizi ya kigaidi ya Israel nchini Qatar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130624-dunia_yalaani_mashambulizi_ya_kigaidi_ya_israel_nchini_qatar
Mashambulizi ya anga ya Israel huko Doha, Qatar, yaliyowalenga viongozi Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, yameendelea kulaaniwa na nchi na viongozi mbali mbali kote duniani.
(last modified 2025-09-10T02:54:46+00:00 )
Sep 10, 2025 02:54 UTC
  • Dunia yalaani mashambulizi ya kigaidi ya Israel nchini Qatar

Mashambulizi ya anga ya Israel huko Doha, Qatar, yaliyowalenga viongozi Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, yameendelea kulaaniwa na nchi na viongozi mbali mbali kote duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali mashambulio hayo ya anga na kuyataja kuwa ni "ukiukwaji mkubwa wa uhuru na mamlaka ya kujitawala Qatar."

Huku akiashiria juu ya nafasi chanya ya Qatar katika upatanishi wa juhudi za kusitisha mapigano huko Gaza na kuwezesha kuachiliwa kwa mateka, Guterres amezitaka pande zote kuweka kipaumbele kwa usitishaji vita wa kudumu badala ya kushadidisha ukosefu wa utulivu wa kikanda.

Nayo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imelielezea shambulio hilo la anga kama ukiukaji wa mamlaka ya Qatar na kitendo cha kuvuruga utulivu, huku ikitaka hatua za pamoja zichukuliwe kuzuia uchokozi zaidi.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV ameelezea wasiwasi wake juu ya shambulio hilo la anga, akibainisha kuwa hali ya eneo la Asia Magharibi ni "mbaya sana", huku akionya kuhusu taathira hasi za uchokozi huo, hasa kwa utulivu wa kikanda.

Naye Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Ismail Baqaei amelaani mashambulizi hayo ya utawala wa kizayuni dhidi ya Qatar na dhidi ya ujumbe wa Hamas na kuyataja kuwa ni hatari kubwa na ukiukaji wa kanuni, malengo na kanuni zilizoainishwa katika Hati ya Umoja wa Mataifa.

Hali kadhalika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imelaani hujuma hiyo na kuliataja kuwa "shambulio la kigaidi" dhidi ya Qatar. Ujumbe huo wa HAMAS uliolengwa ulikuwa umejumuika kujadili mapendekezo ya Marekani ya kusitisha mauaji ya halaiki yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni huko katika Ukanda wa Gaza.