Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lailaani Israel kwa kuishambulia Qatar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130698-baraza_la_usalama_la_umoja_wa_mataifa_lailaani_israel_kwa_kuishambulia_qatar
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani shambulio la Israel dhidi ya mji mkuu wa Qatar, Doha siku ya Jumanne na kutaka kupunguzwa kwa mvutano na taharuki katika eneo.
(last modified 2025-09-12T03:06:26+00:00 )
Sep 12, 2025 03:06 UTC
  • Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lailaani Israel kwa kuishambulia Qatar

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani shambulio la Israel dhidi ya mji mkuu wa Qatar, Doha siku ya Jumanne na kutaka kupunguzwa kwa mvutano na taharuki katika eneo.

Wajumbe wa baraza hilo wametoa taarifa hiyo kabla ya mkutano wa dharura jana Alkhamisi, ambao uliitishwa kujadili mashambulizi ya Israel yaliyowalenga viongozi wa Hamas katika mji mkuu wa Qatar, huku utawala huo wa Kizayuni ukishadidisha mashambulizi yake katika Jiji la Gaza, na kuwalazimisha zaidi ya 200,000 kuyakimbia makazi yao.

Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani ameliambia baraza hilo kwamba, Doha itaendeleza juhudi zake za kibinadamu na kidiplomasia, lakini haitavumilia ukiukaji zaidi wa usalama na mamlaka yake ya kujitawala.

Mashambulizi hayo ya anga ya Israel huko Doha, Qatar, yaliyowalenga viongozi Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, yameendelea kulaaniwa na nchi na viongozi mbali mbali kote duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali mashambulio hayo ya anga na kuyataja kuwa ni "ukiukwaji mkubwa wa uhuru na mamlaka ya kujitawala Qatar."

Naye Rais Masoud Pezeshkian wa Iran ameulaani vikali utawala haramu wa Israel kwa kitendo chake hicho 'haramu, cha kinyama na kinacholenga kuvuruga amani ya eneo,' baada ya utawala huo wa Kizayuni kushambulia ardhi ya Qatar na kuwaua shahidi viongozi kadhaa wa Harakati ya Hamas.

Naye Balozi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa, Amar Bendjama, amesema: "Israeli inafanya kana kwamba hakuna sheria, kana kwamba mipaka ni udanganyifu, kana kwamba mamlaka ya kujitawala ni hoja isiyoweza kuepukika, na kana kwamba Hati ya Umoja wa Mataifa ni maandishi ya zamani."