Mwandishi habari mmoja huaga dunia kila siku nne na nusu
(last modified Thu, 03 Nov 2016 03:53:50 GMT )
Nov 03, 2016 03:53 UTC
  • Mwandishi habari mmoja huaga dunia kila siku nne na nusu

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) llimetangaza kuwa mwandishi habari mmoja duniani hupoteza maisha katika kila siku nne na nusu.

Ripoti iliyochapishwa kufuatia ombi la nchi 39 wanachama wa Baraza la Kiserikali la nchi wanachama wa Unesco limebainisha kuwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita waandishi habari 827 walipoteza maisha  wakiwa kazini. Ripoti hiyo imeendelea kufafanua kuwa, maeneo  hatari zaidi duniani kwa waandishi habari ni katika baadhi ya nchi za Kiarabu kama Syria, Iraq, Yemen na Libya; na kwamba Amerika ya Latini inachukua nafasi ya pili ikitambuliwa kama eneo baya zaidi duniani kwa waandishi habari ikitanguliwa na nchi za Kiarabu zilizotajwa.

Waandishi wa habari wakiwa kazini

Ripoti hiyo imeeleza kuwa asilimia 59 ya waandishi habari waliuawa kati ya mwaka 2006 hadi mwaka jana 2015; ambapo kati ya jumla ya waandishi habari 213 waliouliwa, 78 waliuawa katika nchi za Kiarabu.

Katika ripoti yake hiyo Unesco imeongeza kuwa, waandishi habari wa ndani wako katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha kulinganisha na wa nchi za nje.