Ghasia za uchaguzi Marekani, kadhaa wajeruhiwa California
Huku matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais nchini Marekani yakisubiriwa kwa hamu na shauku, mtu mmoja ameuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika tukio la ufyatuaji risasi lililojiri katika jimbo la California.
Ghasia hizo zilizotokea katika mji wa Azusa, yapata kilomita 40 mashariki mwa mji wa Los Angeles usiku wa kuamkia leo, zimesababishwa kufungwa vituo viwili vya kupigia kura.
Habari zinasema kuwa, mshukiwa aliyehusika na tukio hilo alikuwa amevalia fulana ya kuzuia risasi huku akiwa amejizatiti kwa bunduki, ambapo alianza kufyatua risasi ovyo na kusababisha maafa hayo kabla ya kukabiliwa na maafisa wa polisi.Vyombo vya habari nchini Marekani vimekuwa vikiripoti kushadidi tofauti za kisiasa katika siku za hivi karibuni kiasi cha kuhatarisha usalama wa nchi.
Huku hayo yakiarifiwa, mgombea wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump anaongoza kwa asilimia 49 katika matokeo ya majimbo kadhaa, huku hasimu wake wa Democrat, Hillary Clinton akipata asilimia 47. Trump kwa sasa anaongoza majimbo ya Florida, Alabama, North Carolina, Ohio, Georgia, New Hampshire, Indiana, Arkansas na Kentucky huku Clinton akizoa kura nyingi katika majimbo ya Colorado, Virginia, New York, New Jersey, Delaware, Massachusetts, Maryland, Connecticut na Vermont.
Hata hivyo mbali na kushinda idadi ya kura za wananchi, mgombea wa urais sharti apate angalau kura 270 za wajumbe 538 kutoka majimbo yote 50 ya Marekani ili kuwa rais wa nchi hiyo.
Hadi tunaenda mitamboni, Trump alikuwa na kura 216 za wajumbe hao huku hasimu wake Clinton akiwa na kura 209.