Wademocrat wakosoa sheria ya uchaguzi US baada ya ushindi wa Trump
Seneta mmoja wa chama cha Democrat nchini Marekani ameandaa muswada wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Uchaguzi ya nchi hiyo kufuatia ushindi wa Donald Trump wa chama cha Republican katika uchaguzi wa wiki iliyopita.
Seneta Barbara Boxer amesema sheria hiyo inahitaji kufanyiwa marekebisho ili iendane na matakwa ya wananchi na misingi ya demokrasia. Mwanasiasa huyo wa Democrat amesema miongoni mwa vipengee anavyopendekeza vifanyiwe marekebisho ni Sura ya Pili ya Katiba ambayo imelipa uwezo na mamlaka Jopo la Wajumbe wa Majimbo (Electoral College), kutoa uamuzi wa mwisho katika uchaguzi wa rais nchini humo.
Mgombea wa urais nchini Marekani sharti apate angalau kura 270 za wajumbe 538 kutoka majimbo yote 50 ya nchi ili kuibuka mshindi.
Seneta huyo wa chama cha Democrat amesema jopo la watu wachjache kupewa uwezo wa kuwa na sauti ya mwisho katika uchaguzi wa rais nchini, ni suala lililopitwa na wakati, lisilozingatia misingi ya demokrasia na ambalo haliakisi hali halisi na matakwa ya jamii ya Marekani.
Ikumbukwe kuwa, mgombea wa kiti cha Democrat katika uchaguzi wa rais uliopita Hillary Clinton, alishinda kura za wananchi (popular vote) kwa kupata kura 62,318,079, huku mwenzake wa Republican Donald Trump akipata 61,166,063. Hata hivyo Trump alimshinda Clinton katika kura ya wajumbe wa majimbo ya nchi hiyo, kwa kupata 290 dhidi ya 228.