Maandamano makubwa zaidi dhidi ya serikali ya Uingereza
Maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wahadhiri nchini Uingereza wameshiriki katika maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika mitaa ya mji wa London.
Katika nara na kauli mbiu zao, waandamanaji wamesema badala ya serikali ya Uingereza kupunguza bajeti ya elimu ya juu inapaswa kupungza bajeti yake ya kuunda silaha za nyuklia.
Waandamanaji hao aidha wametoa nara dhidi ya sera za kubana matumizi ya kiuchumi, sera ambazo zimeongeza mashinikizo ya kifedha kwa mfumo wa elimu ya juu huku wakisema ni jambo lisilokubalika kwa serikali kupunguza bajeti ya elimu ya juu.
Maandamano hayo makubwa ya wanafunzi nchini Uingereza ni ishara nyingine ya kuongezeka malalamiko ya umma dhidi ya sera za kiuchumi za serikali ya chama cha Wahafidhina au Conservative.
Baada ya kuondoka madarakani David Cameron, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza na kuchukua madaraka Theresa May, ambaye pia ni wa chama cha Wahafidhina, hakuna mabadiliko yoyote yaliyojiri katika kupunguza au kusitisha sera za kubana matumizi. Pamoja na kubainika madhara ya sera hizo, serikali ya sasa ya Uingereza inasisitiza kuendelea na mchakato huo ulioanzishwa na Cameron na kupuuza malalamiko ya wananchi.
Wanaoathirika zaidi na sera hizo za kubana matumizi ni tabaka la kati katika jamii ya Uingereza, sekta ya elimu ya juu na vyuo vikuu hasa wanachuo Waingereza ambao hawapati msaada wa kutosha wa kifedha na hivyo inabidi wachukue mikopo ili kuendeleza masomo yao.
Serikali ya Wahafidhina nchini Uingereza imeongeza karo ya wanafunzi wa vyuo vikuu na hivyo kupelekea familia nyingi kukumbwa na matatizo katika kuwaelimisha watoto wao. Aidha wanafunzi wanaohitimu masomo ya vyuo vikuu na kupata kazi wanakumbwa na matatizo ya kifedha kwani serikali huyashinikiza mashirika yaliyowaajiri kukata kiasi kikubwa cha fedha katika mishahara yao ili kulipa madeni ya mikopo ya masomo waliyochukua.
Ni kwa sababu hii ndio wanafunzi waliokuwa wakiandamana wakalaani hatua hiyo ya serikali ya Wahafidhina na kuitaja kuwa aibu kubwa.
Serikali ya Uingereza, katika fremu ya sera zake za kubana matumizi imepunguza kwa kiasi kikubwa bajeti yake katika sekta za afya, elimu na huduma nyinginezo kwa wananchi. Hii ni katika hali ambayo serikali hiyo ya London imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya mradi wa 'Trident' wa kukarabati makombora yake ya nyuklia na nyambizi zinazosheheni silaha za nyuklia.
Inakadiriwa kuwa miradi hiyo ya kuboresha silaha za nyuklia itagharimu Pauni bilioni 30 pamoja na Pauni bilioni 10 ambazo zimetajwa kuwa za matumizi yasiyotabirika.
Yamkini bajeti hiyo ikawa kubwa zaidi kuliko ile inayotajwa kwani mwaka 2013, Taasisi ya Huduma za Ufalme wa Uingereza (The Royal United Services Institute) ilitabiri kuwa oparesheni ya kuboresha mfumo wa makombora ya nyuklia itagharimu Pauni bilioni 80 hadi 70. Mwaka 2014 gharama za mradi huo zilikadiriwa kuwa Pauni billioni 100.
Wakosoaji wa mradi huo wakiwemo wanachuo wanaserma serikali ya Wahafahdina ya Uingereza inatumia visingizio vya nakisi ya bajeti kupunguza matumizi katika sekta za elimu, jamii na afya lakini wakati huo huo inatumia mabilioni ya Pauni, fedha za walipa kodi wa Uingereza kuimarisha maghala adhimu ya silaha za nyuklia.
David Cameron Waziri Mkuu wa Uingereza kuanzia mwaka 2010 aliweza kupunguza asilimia 20 ya bajeti ya huduma za umma lakini sera hizo zimepelekea watu wenye pato la chini kukumbwa na matatizo makubwa ya kimaisha.
Hivi sasa serikali mpya ya Theresa May si tu kuwa inaendeleza sera hizo mbovu za Cameron bali pia inalenga kufuta kiasi kikubwa cha bajeti ya afya, huduma za jamii na elimu jambo ambalo litapelekea idadi kubwa ya watu, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, kukumbwa na matatizo makubwa.