Onyo la mkuu wa CIA kwa Trump kuhusu JCPOA
-
John O. Brennan, Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA
John O. Brennan, Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA amemuonya Donald Trump, rais mteule wa Marekani kutokana na msimamo wake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 yanayojulikana kwa jina la JCPOA na kusisitiza kuwa, haitakuwa busara hata kidogo kufutwa makubaliano yaliyotiwa saini na Tehran na Washington.
Amesema, kufutwa makubaliano hayo kutazipelekea nchi nyingine duniani zipate nguvu za kuendelea na miradi yao ya nyuklia. Mkuu huyo wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA aidha amesema: Ninavyoamini mimi kama makubaliano hayo yatafutwa, kutazuka balaa kubwa na hatua hiyo itakuwa haijawahi kuchukuliwa mfano wake katika historia nzima ya Marekani.
Onyo la kiongozi wa ngazi za juu wa masuala ya usalama nchini Marekani kuhusu hatari ya moja ya ahadi kuu za Donald Trump alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi yaani kufuta makukbaliano ya nyuklia ya JCPOA, kwa hakika linadhihirisha wasiwasi ilio nao serikali ya hivi sasa ya Marekani kuhusu utendaji wa serikali ijayo ya nchi hiyo. Ni wazi kuwa, iwapo Trump ataamua kufuta au kufanyia marekebisho makubaliaho ya JCPOA ambayo yamefikiwa baada ya juhudi kubwa za kimataifa, kutaipotezea heshima na itibari Marekani. Fauka ya hayo ni kuwa, makubaliano ya JCPOA si makubaliano ya pande mbili za Marekani na Iran bali Marekani ni sehemu tu ya nchi sita kubwa duniani zilizofikia makubaliano hayo na Iran.
Ukitoa Marekani, kuna nchi nyingine tatu za Ulaya waitifaki wa Marekani zilizoshiriki kikamilifu kwenye mazungumzo yaliyozaa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA nazo ni Uingereza, Ufaransa na Ujerumaini. Nchi nyingine kubwa zilizotia saini makubaliano hayo ni Russia na China. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo lilishiriki kikamilifu kwenye ufanikishaji wa makubaliano hayo na mwezi Julai 2015, lilipitisha azimio nambari 2231 la kupasisha utekelezaji wa makubaliano hayo. Makubaliano hayo yaliyopata baraka kamili za kimataifa yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016 na tangu wakati huo, Iran imetekeleza kikamilifu ahadi zake zote na hilo limethibitishwa na ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA. Kwa upande wa nchi za Ulaya pia, kutokana na matatizo yao mbalimbali ya kiuchumi, zimeonesha hamu kubwa ya kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi na kibiashara na Iran, hivyo nazo zimeamua kutilia mkazo uhakika kuwa Iran imechukua hatua zinazotakiwa kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA, na hazifurahishwi na ukwamishaji wa kila namna unaowekwa na Marekani katika utekelezaji wa makubaliano hayo. Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya Federica Mogherini alisema katikati ya mwezi huu wa Novemba, baada ya Donald Trump kutangazwa mshindi wa urais wa Marekani kwamba, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA si makubaliano ya pande mbili za Tehran na Washington, bali ni makubaliano ya pande kadhaa, na ni yenye nguvu za maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hivyo Trump hawezi kuyavuruga.
Kwa kutilia maana hayo tunaweza kusema kuwa, iwapo Trump ataamua kutekeleza ahadi zake za wakati wa kampeni za uchaguzi, za kufuta makubaliano ya JCPOA, basi ajiweke tayari kukabiliana na radiamali na majibu makali kutoka kwa waitifaki wa Washington wa barani Ulaya. Si hayo tu, lakini pia hatua hiyo itazidi kuiondolea Marekani heshima ya kisiasa duniani kwani watu wote ulimwenguni wataona kuwa watawala wapya wa Marekani si watu wa kuaminika na wamedharau hata makubaliano ya kimataifa ambayo serikali yenyewe ya Marekani imeyatia saini kwa ridhaa yake yenyewe. Vile vile onyo lililotolewa na Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA kwa Trump kuhusu madhara makubwa ya kufuta makubaliano ya JCPOA linaonesha namna wasiwasi ulivyotanda katika ngazi za juu za utawala nchini Marekani. John O. Brennan amemwambia wazi Trump kuwa kufuta makubaliano ya JCPOA si tu kutaipotezea itibari Marekani kimataifa na kuionesha kuwa ni nchi isiyo na mwamana, lakini pia nchi nyinginezo duniani nazo zitapata nguvu kwa kuendelea na miradi yao ya nyuklia na hazitakuwa tayari kusikiliza ahadi zisizo na dhamana ya kutekelezwa. Hali ikiwa hivyo, bila ya shaka yoyote itapelekea kuongezeka wasiwasi na hatari ya nyuklia katika kona zote dunia.