Kansela wa Ujerumani ataka kupigwa marufuku burqa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20923-kansela_wa_ujerumani_ataka_kupigwa_marufuku_burqa
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa kupigwa marufuku vazi la stara la burqa, linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 07, 2016 07:19 UTC
  • Kansela wa Ujerumani ataka kupigwa marufuku burqa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa kupigwa marufuku vazi la stara la burqa, linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu.

Akizungumza hapo jana mjini Essen wakati akizindua azma yake ya kuwania muhla mwingine wa uenyekiti wa muungano wa Kikristo unaojulikana kama Christian Democratic Union (CDU), Merkel alisema vazi hilo la niqabu linafaa kupigwa marufuku nchini humo akisisitiza kuwa Sheria ya Ujerumani iko juu ya kanuni na sheria za kidini.

Amesema usalama, haki na sheria ni misingi mikuu ya muungano wa CDU na kusisitiza kuwa, Wajerumani wa asili na wale waliongia nchini humo hivi karibuni akikusudia wahajiri, wanafaa kufuatwa sheria za nchi hiyo kikamilifu.

Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani

Matamshi ya Angela Merkel, yanajiri siku chache baada ya Bunge la Uholanzi kupasisha muswada wa kutaka kupigwa marufuku vazi hilo la staha.

Iwapo Bunge la Seneti la Uholanzi litaidhinisha sheria hiyo, yeyote atakayevaa vazi hilo la stara katika maeneo ya umma atatozwa faini ya Euro 405 sawa na dola 430 za Marekani.

Mapema mwezi Oktoba mwaka huu, Bulgaria ilijiunga na baadhi ya nchi za Magharibi zilizopiga marufuku vazi la burqa kama vile Canada, Ubelgiji na Ufaransa, baada ya bunge la nchi hiyo kupasisha sheria inayopiga marufuku vazi hilo linalovaliwa na wanawake Waislamu nchini kote.