Iran: Itibari ya JCPOA inategemea kuheshimiwa makubaliano hayo na pande zote
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21331-iran_itibari_ya_jcpoa_inategemea_kuheshimiwa_makubaliano_hayo_na_pande_zote
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kufanikiwa makubaliano ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi za kundi la 5+1 kunategemea iwapo pande zote zitayaheshimu na kuyatekeleza makubaliano hayo ipasavyo au la.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 13, 2016 04:39 UTC
  • Iran: Itibari ya JCPOA inategemea kuheshimiwa makubaliano hayo na pande zote

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kufanikiwa makubaliano ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi za kundi la 5+1 kunategemea iwapo pande zote zitayaheshimu na kuyatekeleza makubaliano hayo ipasavyo au la.

Gholam-Ali Khoshroo, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa aliyasema hayo jana Jumatatu mbele ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, uliojadili ripoti ya Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki IAEA.

Amesema katika hali ambayo IAEA na pande zote za makubaliano hayo ya nyuklia zimethibitisha kuwa Iran imetekeleza kikamilifu mapatano hayo, kila mmoja hana budi kufungamana na mapatano hayo pasina kufanya vitendo vyovyote vinavyoashiria kuwa anakengeuka wajibu wake.

Katibu Mkuu anayeondoka wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

Kabla ya kushiriki mkutano huo wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa, Khoshroo alikabidhi barua ya malalamiko ya Jamhuri ya Kiislamu, kuhusu hatua ya Kongresi ya Marekani kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran.

Hivi karibuni Rais Hassan Rouhani alisema kuwa Iran haitairuhusu Marekani ikiuke au ichane hati ya makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kwamba, Washington haiwezi kuathiri irada, kusimama imara wala muqawama wa taifa la Iran.

Aidha Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) nao wamelaani hatua ya wajumbe wa Bunge la Kongresi la Marekani ya kurefusha kwa muda wa miaka 10 sheria ya kuiwekea Iran vikwazo na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua mwafaka zinazoendana na hatua hiyo ya Washington.

Viongozi wa dunia walioshuhudia kusainiwa makubaliano ya nyuklia mjini Vienna Julai 2015