Arab League yatahadharisha kuhusu kuhamishiwa ubalozi wa Marekani huko Baitul Muqaddas
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ametoa indhari kuhusu harakati zinazotekelezwa na serikali mpya ya Marekani za kutaka kuuhamishia ubalozi wake huko Baitul Muqaddas.
Ahmad Abul Ghait Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema kuwa kitendo cha kuuhamishia ubalozi wa Marekani huko Baitul Muqaddas kitakuwa na taathira hasi kwa ufumbuzi wa kadhia ya Palestina. Katibu Mkuuu wa Arab League ameyatamka hayo huko Cairo mji mkuu wa Misri katika mazungumzo kati yake na ujumbe wa Kongamano la Wananchi wa Quds chini ya uongozi wa Bilal al Natisha. Abul Ghait ameongeza kuwa suala la kutaka kuuhamisha ubalozi wa Marekani na kuupeleka Baitul Muqaddas limearifiwa kwa idara husika za sekretarieti ya Arab League ili kuchunguzwa na kuona ni kwa namna gani wataweza kukabiliana na muamala huo wa Marekani.
Itakumbukwa kuwa Rais Mteule wa Marekani Donald Trump aliahidi katika kampeni zake za kuwania kiti cha rais kuwa atauhamisha ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv na kuupeleka Baitul Muqaddas.
Hii ni katika hali ambayo nchi nyingi zikiwemo za Ulaya hadi sasa zimejizuia kuchukua hatua ya kuunga mkono kuhamishiwa ubalozi wa Marekani huko Baitul Muqaddas kwa kuhofia radiamali zitakazopata kutoka kwa fikra za waliowengi. Kitendo cha Marekani kulivalia njuga suala hilo kinadhihirisha namna serikali ijayo ya nchi hiyo inavyouzingatia utawala wa Kizayuni chini ya kivuli cha ukaliaji mabavu, kughusubu na jinai kubwa za utawala huo dhidi ya Wapalestina.