Russia: Wamagharibi wanakwamisha mapambano dhidi ya ugaidi wa silaha za kemikali
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zinakwamisha mapambano halisi dhidi ya ugaidi wa silaha za kemikali kwa kuingiza masuala ya siasa katika kadhia ya utumiaji wa silaha za aina hiyo nchini Syria.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema kuwa ushahidi usio na shaka unathibitisha kuwa, makundi ya kigaidi yametumia silaha za kemikali nchini Syria. Zakharova ameongeza kuwa, msimamo wa nchi za Magharibi kuhusu utumiaji wa silaha za kemikali nchini Syria na kutoyalaani makundi ya kigaidi yaliyotumia silaha hizo ni kinyume na mantiki na akili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia amesema kuwa, Ufaransa, Uingereza na Marekani zinanyamazia kimya kwa makusudi jinai za silaha za kemikali zinazotumiwa na makundi ya kigaidi nchini Syria hususan kundi la Daesh.
Maelfu ya watu wanaripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyofanywa na makundi ya kigaidi hususan Daesh katika maeneo kadhaa ya Syria.