Mmarekani mweusi afukuzwa katika mkutano wa Trump
Mgombea wa kiti cha rais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Dolad Trump amemfukuza mwanamke mmoja mweusi wa nchi hiyo katika mkutano wake wa kampeni.
Trump ambaye anaongoza katika mbio za kuwania tiketi ya kubeba bendera ya Republican katika uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani jana alimfukuza mwanamke mmoja Mmarekani mwenye asili ya Afrika katika mkutano wake baada ya raia huyo kulalamika dhidi ya siasa na matamshi ya mwanasiasa huyo bilionea. Trump aliwataka wafuasi wake kumfukuzia mbali mwanamke huyo na mara moja mashabiki wa Trump walimsukuma na kumtoa nje ya eneo la mkutano kwa mabavu.
Mkutano mwingine wa kampeni za uchaguzi wa Donald Trump uliofanyika Jumatatu iliyopita katika Chuo Kikuu cha Radford jimboni Virginia pia ulikabiliwa na malalamiko na upinzani mkubwa wa Wamarekani wasio wazungu.
Matamshi ya kichochezi na dharau yanayotolewa na mwanasiasa huyo dhidi ya Wamarekani weusi yamezusha hasira kubwa nchini humo.