Mfuasi wa Trump amshambulia mwanamke Mwislamu New York
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24335-mfuasi_wa_trump_amshambulia_mwanamke_mwislamu_new_york
Katika tukio jingine linalothibitisha kuwa uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Waislamu umeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Marekani, mfuasi wa Rais mpya wa nchi hiyo Donald Trump kutoka Massachusetts amemshambulia na kumjeruhi mwanamke Mwislamu katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa John F. Kennedy mjini New York.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2017 23:18 UTC
  • Mfuasi wa Trump amshambulia mwanamke Mwislamu New York

Katika tukio jingine linalothibitisha kuwa uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Waislamu umeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Marekani, mfuasi wa Rais mpya wa nchi hiyo Donald Trump kutoka Massachusetts amemshambulia na kumjeruhi mwanamke Mwislamu katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa John F. Kennedy mjini New York.

Mshambuliaji huyo kwa jina Robin Rhodes anaripotiwa kumtupia cheche za maneno makali na hata kumpiga teke mwanamke huyo aliyetambulika kama Rabeeya Khan, mfanyakazi wa shirika la ndege la Delta Airline.

Mashuhuda wanasema kuwa, mtu huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu amemfokea mwanamke huyo na kumwambia: "Trump yuko hapa sasa, atawamaliza nyote. Waulizeni Wajerumani, Wabelgiji na Wafaransa kuhusu hawa watu. Ulivyojifunika kichwa na uso hatuwezi kujua kama wewe ni mwanamme au mwanamke." 

Ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu Marekani

Mwezi uliopita, raia mmoja wa nchi hiyo wa dini ya Kiislamu aliuawa nje ya msikiti jimboni California katika tukio jingine linalodhihirisha chuki dhidi ya Uislamu nchini humo. Mwezi huo huo, Ilhan Omar, Mbunge wa kwanza mwenye asili ya Kisomali kuchaguliwa nchini Marekani alisema dereva mmoja wa teksi alimdhalilisha na kumtolea maneno ya chuki dhidi ya Uislamu mjini Washington. Itakumbukwa kuwa, Septemba mwaka jana, Kituo cha Kiislamu katika jimbo la Florida Marekani kiliteketezwa moto na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu. Baada ya hapo Masjidul Karim wa mji wa Providence huko Rhode Island nchini Marekani ulitumiwa barua yenye chuki za kidini dhidi ya Waislamu.

Ripoti ya hivi karibuni ya Taasisi ya Uchunguzi wa Uhalifu katika jamii ya Marekani inaonesha kuwa, uhalifu wa kawaida umeongezeka kwa karibu asilimia sita nchini Marekani, lakini vitendo vya kihalifu vinavyotokana na chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka kwa asilimia 89.