Trump asaini amri ya kupiga marufuku Waislamu kuingia Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani ametia saini amri ya kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo ambapo hivi sasa kutakuwa na vizingiti kwa wahamiaji na wakimbizi kwa lengo la kuwazuia watu aliowataja kuwa, 'magaidi wa Kiislamu wenye misimamo mikali' kuingia katika nchi hiyo.
Akizungumza Ijumaa baada ya kutia saini amri hiyo inayoonyesha uhasama na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, Trump alitaja utiwaji saini sheria hiyo kuwa hatua kubwa ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu yaliyomo.
Rasimu iliyovuja ya sheria hiyo inaonyesha kuwa, wakimbizi kutoka Syria watazuiwa kuingia Marekani huku wahajiri kutoka nchi za Waislamu kama vile Sudan, Somalia, Iraq, Iran, Libya na Yemen wakipigwa marufuku kwa muda kuingia Marekani.
Wakati wa kampeni zake, Trump alikuwa ametaka Waislamu wazuiwe kikamilifu kuingia Marekani huku kukiwa na taarifa kuwa, rais huyo wa ameanza kutekeleza mpango wa kuwasajili Waislamu wote Marekani kwa lengo la kudhibiti nyendo zao.
Hatua hiyo tata ya Trump ya kuwazuia Waislamu kuingia Marekani imelalamikiwa vikali nchini humo na kote duniani.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na gazeti la Washington Post, karibu asilimia 60 ya Wamarekani hawaridhishwi na utendaji kazi wa Trump.
Ijumaa pia Trump alitia saini sheria mpya ya 'kuimarisha Jeshi la Marekani' ambapo jeshi hilo litapata suhula mpya kama vile ndege za kivita, manowari nk.