Dunia yalaani hatua ya Trump kuwazuia Waislamu kuingia Marekani
Hatua ya rais Donald Trump kuwazuia wahamiaji Waislamu kuingia nchini humo inaendelea kulaani na kukoslewa kote duniani na Marekani kwenywe.
Taasisi mbali mbali za kimataifa zimeitaja hatua hiyo ya Trump ya kuwazui Waislamu kutoka baadhi ya nchi kuingia Marekani ni ubaguzi wa rangi na dhidi ya ubinadmau.
Katika taarifa, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM yametoa taarifa yakitaka Marekani iendelee kuwapokea wakimbizi na wahajiri. Pia Mashirika hayo yamesema yanaamini kuwa wakimbizi wanastahili kutendewa usawa katika kupata ulinzi, msaada na fursa za kupewa makazi bila kujali dini, utaifa au rangi.
Nchi za Iraq, Yemen na Somalia ambazo raia wake wameathiriwa na hatua hiyo zimetoa taarifa na kulaani uamuzi wa kuwazui raia wao Waislamu kuingia Marekani. Harakati ya Ansarullah ya Yemen imelaani hatua ya Marekani kuwataja raia wao nchi hiyo kuwa eti ni magaidi.
Wabunge nchini Iraq pia wamelaani hatua hiyo ya Marekani na kusema watachunguza upya uhusiano wao na Marekani katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS.
Naye mwanariadha maarufu wa Somalia, Mohammad Farah ambaye pia ana uraia pacha wa Uingereza na Somalia na ambaye anamiliki nyumba Marekani inakoishi familia yake amesema atalazimika kuwaambia watoto wake kuwa, 'kutokana na amri ya Trump baba hawezi kuja nyumbani. Aidha amelaani hatua hiyo ya Trump ya kuwapiga mafurufu Waislamu Marekani na kuitaja kuwa ya kijinga.
Wakati huo huo Baraza la Mahusiano ya Kiislamu-Marekani, CAIR, ambalo hutetea haki za Waislamu Marekani, limesema litawasilisha kesi mahakamani kupinga marufuku hiyo ya Trump.
Itakumbukwa kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani Ijumaa alitia saini amri ya kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo ambapo hivi sasa kutakuwa na vizingiti kwa wahamiaji na wakimbizi kwa lengo la kuwazuia watu aliowataja kuwa, 'magaidi wa Kiislamu wenye misimamo mikali' kuingia katika nchi hiyo.