Hujuma za Marekani nchini Yemen zaua watu zaidi ya 50
Makumi ya watu wameuawa katika wimbi jipya la hujuma za ardhini na angani za makomandoo wa Marekani katika mkoa wa Bayda nchini Yemen.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, watu zaidi ya 57 akthari yao wakiwa ni raia wa kawaida wameuawa katika mashambulizi hayo, yaliyofanywa na jeshi la Marekani katika kijiji cha Yakla wilayani Qifah.
Habari zinasema kuwa, operesheni hiyo ilianza nyakati za alfajiri, wakati ambapo drone za Marekani zilipolenga nyumbani kwa kamanda mkuu wa kundi la kigaidi la al-Qaeda, Abdulraoof al-Dhahab na makabiliano makali yakashuhudiwa kati ya wanajeshi hao wa US na wanamgambo wa al-Qaeda.
Vyombo ya habari vya Saudia vimedai kuwa ni raia 16 pekee ndio waliouawa katika hujuma hiyo, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.

Wakati huo huo, kanali ya televisheni ya al-Masirah imeripoti kuwa, mamluki kadhaa wa Saudi Arabia wameuawa katika shambulizi lililotajwa kuwa la kimakosa la Riyadh katika vijiji vya al-Quraishyah na Sharyah mkoani Bayda.
Tokea mwezi Machi mwaka 2015 Saudia imekuwa ikishambulia kijeshi na kuizingira Yemen tokea nchi kavu, angani na baharini kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdurabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kisha kukimbilia usalama wake nchini Saudia.
Pamoja na hayo, mashambulio hayo hayajakuwa na natija nyingine ghairi ya kusababisha maafa ya Wayemen 11,400, kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine, kufanya mamilioni kuwa wakimbizi na kuharibu kabisa miundombinu ya nchi hiyo.