Kushadidi ukatili wa polisi na kamatakamata kote Ufaransa
Siku chache zilizopita maafisa wa polisi Ufaransa walimkamata mwanaume mwenye asili ya Afrika na kumpiga vibaya na baada ya hapo kumnajisi kwa kijiti sambamba na kumvunjia heshimana katika viunga vya mji wa Paris.
Ukatili na unyama huo wa polisi umepelekea kuibuka maandamano na machafuko kwa usiku wa tano mfululizo kaskazini mwa Paris na viunga vyake. Waandamanaji mbali na kulaani vikali ukatili wa polisi na namna wanavyotumia vibaya mamlaka yao, wametaka uadilifu utendeke.
Katika maandamano hayo, polisi mjini Paris wameendeleza ukatili na utumiaji mabavu kwa kuwakamata mamia ya vijana waliokuwa wakiandamana. Kufuatia kuendelea unyama huo wa polisi, vijana waliokuwa na hasira wameteketeza moto magari na kuvamia maduka kadhaa.
Maandamano ya kulalamikia ukatili wa polisi yanazidi kuenea katika maeneo mengi ya kaskazini mwa mji mkuu Paris.
Duru zinaarifu kuwa Alhamisi iliyopita katika mtaa wa Aulnay-sous-Bois, kijana huyo mwenye asili ya Afrika, aliyetambuliwa kwa jina la kwanza la Theo, na ambaye ana umri wa miaka 22 alikamatwa na maafisa wanne wa polisi ambao walimtandika vibaya kabla ya kumnajisi kwa kijiti na kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata katika ukatili huo amelazimika kufanyiwa upasuaji hospitalini. Ukatili huo wa aina yake ndicho chanzo cha machafuko na malalamiko ya sasa mjini Paris na serikali ya nchi hiyo inajaribu kutumia mbinu mbali mbali kutuliza hasira za wananchi.

Ni kwa msingi huo ndio Waziri Mkuu wa Ufaransa Bernard Cazeneuve na Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo wakataka maafisa wa polisi waliohusika na kitendo hicho cha kinyama kufikishwa kizimbani. Rais Francois Hollande wa Ufaransa naye pia katika kujaribu kutuliza hasira za wananchi amemtembelea kijana huyo mwenye asili ya Afrika katika hospitali na kukaa pembeni yake kwa muda wa nusu saa.
Pamoja na hatua hizo lakini waandamanaji wameendelea kulalamikia ukatili na utovu wa maadili katika polisi ya Ufaransa. Maandamano hayo yanazidi kuenea na kuna uwezekano yakawa mabaya kama yale ya 2005. Maandamano ya sasa pia yanaashiria namna wahajiri nchini Ufaransa wanavyoendelea kubaguliwa huku kukiwa na idadi kubwa ya wasio na ajira wala matumaini maishani miongoni mwao.
Mwaka jana pia, baada ya polisi ya Ufaransa kumkamata kijana aliyekuwa na umri wa miaka 24 na kisha kupoteza maisha akiwa kizuizini, kulizuka maandamano makubwa na ghasia kote katika nchi hiyo ya Ulaya ambapo polisi walitumia mabavu dhidi ya waandamanaji.
Pamoja na kuwa nchi za Ulaya na Marekani zinadai kutetea na kuheshimu haki za binadamu lakini tunashuhudia namna ambavyo Waislamu na watu wenye asili ya Afrika wanavyobaguliwa, kuteswa na kukandamizwa katika nchi hizo za Magharibi
Katika miaka ya hivi karibuni nchini Marekani polisi wamewaua kiholela na kuwakamata kinyume cha sheria vijana kadhaa wenye asili ya Afrika jambo ambalo limeibua maandamano makubwa katika miji mikubwa ya nchi hiyo.

Kutokana na ukatili huo wa polisi, hivi sasa nchini Marekani kumeibuka harakati inayojulikana kama "Maisha ya Watu Weusi Ni Muhimu Pia" (Black Lives Matter). Tawi la Ufaransa la harakati hiyo ndilo linaongoza maandamano ya kulalamikia kunajisiwa kijana huyo mweusi mikononi mwa polisi wazungu.
Ahadi hewa za wakuu wa Ufaransa kuwa watazuia ukatili wa polisi zinatolewa pasina kuchukuliwa hatua zozote za kivitendo na hali hiyo imezidisha hasira za wananchi ambao sasa wanataka kuona uadilifu na haki ikitendeka.