Msomi wa Algeria: Ni Iran pekee inayohuisha kadhia ya Palesina duniani
Msomi na mtafiti wa nchini Algeria sambamba na kupongeza hotuba ya hivi karibuni ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kongamano la kimataifa la kuunga mkono Intifadha ya Palestina hapa mjini Tehran kwa kuitaja kama kadhia ya Palestina kama maudhui kuu ya ulimwengu wa Kiislamu, amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee duniani ambayo imeweza kuhuisha kadhia hiyo.
Idah Falahi, msomi na mshauri wa zamani wa vyombo vya habari katika Wizara ya Masuala ya Dini na Wakfu nchini Algeria ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA na kuongeza kuwa, hotuba ya Ayatullah Ali Khamenei katika kongamano hilo lililomalizika hivi karibuni mjini Tehran, iliainisha njia ya Intifadha ya Palestina katika hatua ijayo kama ambavyo pia ililitaja suala la Palestina kama kadhia kuu ya ulimwengu wa Kiislamu. Falahi ameongeza kuwa, baadhi ya watawala wa Kiarabu wamelifanya suala la Palestina kuwa la upande fulani tu na kwamba Waarabu hao kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni wanazuia mafanikio ya Intifadha hiyo.

Msomi huyo na mtafiti wa nchini Algeria amepongeza sana hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuitisha kongamano hilo alilolitaja kuwa 'Mkutano wa Kipekee' na kusisitiza kuwa, mkutano huo ulishabihiana sana na ibada ya Hijjah isipokuwa tu kwamba ulihudhuriwa na Waislamu, Wakristo, Mayahudi na watu wa kaumu tofauti wanaopinga Uzayuni kutoka maeneo tofauti ya dunia. Falahi amesisitiza kuwa kila mwanadamu sawa sawa awe anakubaliana na Iran au la anakiri kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio nchi pekee duniani ambayo imeweza kuhuisha kadhia ya Palestina. Zaidi ya jumbe 80 na wageni 700 kutoka nchi tofauti za dunia walishiriki katika mkutano huo wa kimataifa wa sita kwa ajili ya kuunga mkono Intifadha ya Palestina, ulioanza tarehe 21 hadi 22 hapa mjini Tehran.