Wafuasi na wapinzani wa Trump watwangana makonde nchini Marekani
Habari kutoka nchini Marekani zinasema kuwa kumezuka mapigano baina ya wafuasi na wapinzani wa Donald Trump katika mji wa Berkeley wa jimbo la California, magharibi mwa nchi hiyo.
Televisheni ya Russia Today imeripoti habari hiyo na kusema kuwa, mapigano hayo makali yamezuka kwenye maandamano ya wafuasi na wapinzani wa Donald Trump huku baadhi ya waandamanaji wakitumia mabomu ya moto dhidi ya wapinzani wao.
Watu kadhaa wamejeruhiwa kwenye mapigano hayo ambapo kwa mujibu wa watu walioshuhudia, polisi hawakuchukua hatua yoyote kuyazuia.
California ni jimbo ambalo viongozi wake wamekuwa wakifanya juhudi za kuwa huru katika siasa zao kuhusu wahamiaji na kutofautiana na siasa za serikali kuu inayoongozwa na Donald Trump.
Wapinzani wa siasa za Donald Trump wanamtuhumu rais huyo wa Marekani kuwa ni mbaguzi wa rangi mwenye chuki na watu wasio Wazungu.
Idadi ya wapinzani wa siasa hizo za Donald Trump wanaongezeka siku hadi siku ndani na nje ya Marekani na wanasema kuwa, tangu aingie madarakani huko Marekani, Trump amepelekea kuzuka machafuko na hali ya wasiwasi mkubwa ndani ya jamii ya Marekani na duniani kiujumla.