Utafiti: Vijana wengi Marekani wanasema Trump si rais halali
(last modified Sun, 19 Mar 2017 07:18:28 GMT )
Mar 19, 2017 07:18 UTC
  • Utafiti: Vijana wengi Marekani wanasema Trump si rais halali

Utafiti unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya vijana wa Marekani wanamtazama Donald Trump kama rais ambaye si halali, mpuuzi na asiyekuwa na haiba ya uongozi.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la GenForward na matokeo yake kuchapishwa na shirika la habari la AP jana Jumamosi umeonyesha kuwa, asilimia 57 ya vijana nchini Marekani wanahisi kuwa Trump ni 'rais haramu na asiyefaa'.

Utafiti huo umebainisha kuwa, asilimia 75 ya vijana wa Marekani wenye asili ya Afrika na asilimia 50 ya vijana weupe wa Kimarekani wanahisi kuwa Trump ni rais asiyejiheshimu.

Maandamano dhidi ya Trump nchini Marekani yalianza siku ya kuapishwa kwake

Kwa mujibu wa utafiti huo wa shirika la GenForward, vijana wanane kati ya kumi nchini Marekani hawakubaliani na sera za Trump na mfumo wake wa uongozi.

Utafiti mwingine uliofanywa na Chuo Kikuu cha Quinnipiac huko Connecticut nchini Marekani ulisema kuwa, asilimia 63 ya wapiga kura Marekani wanasema kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la chuki na taasubi tokea Trump achaguliwe Novemba 2016 huku asilimia 32 wakiamini kuwa hakuna chochote kilichobadilika. 

Tags