Marekani na Uingereza zawabana zaidi wasafiri kutoka nchi kadhaa za Waislamu
Serikali ya Marekani jana Jumanne ilipiga marufuku wasafiri kutoka nchi 8 za Waislamu kuingia katika ndege zinazoelekea nchini humo wakiwa na zana za electroniki kubwa zaidi ya simu za kiganjani. Nchi hizo 8 za Waislamu ni Jordan, Misri, Uturuki, Saudi Arabia, Kuwait, Morocco, Qatar na Imarati.
Serikali ya Uingereza pia imetoa amri inayowataka wasafiri kutoka nchi 6 za Waislamu yaani Jordan, Uturuki, Misri, Saudi Arabia, Lebanon na Tunisia wajiepushe kuingia katika ndege zinazoelekea nchini humo wakiwa na simu kubwa za mkononi, laptop na tablet.
Vizingiti hivyo vipya kwa wasafiri kutoka nchi za Waislamu kwa hakika ni sehemu ya siasa na sera mpya za kuzidisha mashinikizo na mbinyo dhidi ya Waislamu ili kuwazuia kusafiri au kuishi katika nchi za Uingereza na Marekani. Kama ilivyokuwa huko nyuma, kisingizio kilichotumiwa kuhalalisha hatua hiyo ni kukabiliana eti na vitisho vya ugaidi. Vilevile afisa mmoja wa serikali ya Marekani amedai kuwa, kwa mujibu wa ripoti za kiusalama, magaidi sasa wanalenga ndege za kusafirisha abiria na za kibiashara na wanabuni mbinu mpya kwa ajili ya kufanya mashambulizi ya aina hiyo. Serikali ya London pia imeamua kufuata kibubusa sera na siasa za Washington katika uwanja huo.
Hatua ya nchi hizo za Magharibi mbali na kuwa ni ubaguzi dhidi ya Waislamu kutokana na ukweli kwamba, ugaidi haujui dini, taifa wala rangi ya mtu, lakini pia uamuzi huo utazidisha hofu na anga ya kuwaogopa Waislamu katika nchi za Magharibi. Kwa maneno mengine ni kuwa, hatua hiyo ni aina fulani ya kusadikisha mtazamo wa Kimagharibi unaodai kuwa, kimsingi Waislamu ni watu hatari sana na tishio kubwa ambao inadili zichukuliwe hatua makhsusi za kukabiliana nao! Picha na propaganda hizi zisizo za kweli hazitakuwa hatua ya mwisho ya nchi za Magharibi dhidi ya Waislamu.
Itakumbukwa kuwa Rais mpya wa Marekani, Donald Trump muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani alitoa amri mbili zilizowapiga marufuku raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kuingia Marekani, suala ambalo limepingwa vikali ndani ya nje ya nchi hiyo. Si hayo tu bali ndani ya Marekani kwenyewe maafisa na wanasheria wamelazimika kwenda mahakamani kutoa changamoto dhidi ya amri hizo za Trump. Kiongozi huyo ambaye ni mashuhuri kwa kuwachukia Waislamu hata kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani, anadai kuwa, kuingia Waislamu nchini humo kunazidisha uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kigaidi! Matamshi na misimamo kama hiyo ya Rais wa Marekani dhidi ya Uislamu inatumiwa na makundi ya kibaguzi ya mrengo wa kulia kwa ajili ya kushambulia misikiti, taasisi na vituo vya Kiislamu.
Jambo muhimu la kuashiria hapa kuhusu propaganda chafu za Wamagharibi kuhusu Uislamu ni kuwa idadi ndogo sana ya Waislamu ndio wenye misimamo ya kuchupa mipaka na aghlabu ya Waislamu kote duniani wanapinga na kuchukia vitendo vinavyofanywa na watu wa kundi hilo potofu. Kwa kutilia maanani ukweli huo, je ni sahihi kweli kuyahusisha matendo yanayofanywa na kundi hilo dogo ambalo si chochote wala lolote na umma mzima wa Waislamu?
Hatua za Marekani na Uingereza dhidi ya wahajiri na wasafiri Waislamu ni sawa na kutoa adhabu kwa umma mzima kwa kosa lililofanywa na idadi ndogo tu ya watu, suala ambalo linapingana na uadilifu na insafu na ni ubaguzi dhidi ya Waislamu.