Asilimia 60 ya Waislamu Marekani wanabaguliwa
Uchunguzi mpya wa maoni umebaini kuwa asilimia 60 ya Waislamu nchini Marekani wamebaguliwa kwa njia moja au nyingine katika kipindi cha mwaka moja uliopita.
Kwa mujibu wa utafiti wa maoni uliofanywa na Shirika na Taasisi ya Sera za Maelewano ya Kijamii katika kipindi hicho Waislamu wamebaguliwa zaidi ya wafuasi wa dini nyingine.
Uchunguzi huo wa maoni pia umebaini kuwa, asilimia 38 ya Waislamu nchini Marekani wana hofu kuhusu usalama wao binafsi kufuatia matokeo ya uchaguzi wa rais mwaka 2016 uliomleta madarakni Donald Trump.
Waislamu wanaishi katika woga wa kuhujumiwa na wazungu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Halikadhalika asilimia 30 ya Waislamu Wamarekani wameripoti kusimamishwa na kukaguliwa zaidi wakiwa katika safari za kimataifa. Watoto Waislamu pia hawajanusurika kwani wengi wanabaguliwa na kubughudhiwa mashuleni kwa ajili ya dini yao. Asilimia 42 ya wanafunzi Waislamu katika shule za msingi na sekondari nchini Marekani wameripoti kusumbuliwa shuleni kwa ajili ya itikadi yao ya Kiislamu katika kipindi cha mwaka moja uliopita.
Wanawake Waislamu ambao huvaa Hijabu pia wamelengwa hadharani nchini Marekani na kati ya kila wanawake watano, mmoja wao amelazimika kupata matibabu baada ya kujeruhiwa katika hujuma zinazotekelezwa na wenye chuki dhidi ya Uislamu.
Uchunguzi huo wa maoni ulifanyika Januari 2017 na kuwashirikisha watu 2,370 wakiwemo Waislamu, Mayahudi, Wakristo Waprotestanti na Wakatoliki.