Kikao cha Brussels cha mawaziri wa mambo ya nje wa NATO
Kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa shirika la kujihami la kijeshi la NATO kilifanyika siku ya Ijumaa iliyopita katika makao makuu ya shirika hilo mjini Brussels, Ubelgiji.
Moja ya maudhui kuu zilizojadiliwa kwenye kikao hicho ni kuendelea hitilafu na tofauti zilizopo baina ya NATO na Russia. Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, alisema kuhusiana na suala hilo kwamba, shirika hilo la kijeshi linahitilafiana kimtazamo na Russia juu ya mambo mengi; na kwa mujibu wa Stoltenberg kutofanya mazungumzo na Moscow kuhusiana na hitilafu zilizopo kunaifanya NATO iendeleze mwenendo huo.
Katika miaka ya karibuni, shirika la kijeshi la NATO na Russia zimekuwa zikihitilafiana juu ya masuala tofauti kuanzia kuendelea kuwekwa mfumo wa ngao ya makombora katika Ulaya Mashariki mpaka katika kadhia ya kuendelezwa sera za kujipanua kijeshi NATO kuelekea upande wa mashariki mwa bara hilo. Pamoja na hayo kuanzia mwaka 2014, sambamba na kupamba moto mgogoro wa Ukraine, ndipo mvutano kati ya Russia na NATO ulipofikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
NATO inaituhumu Russia kuwa inaingilia masuala ya ndani ya Ukraine, lakini viongozi wa Moscow wamekuwa wakisisitiza kila mara kuwa hawajaingilia mapigano yanayojiri mashariki mwa nchi hiyo. Lakini si wanachama wa Ulaya pekee wa NATO wanaolalamikia hatua za Russia katika mgogoro wa Ukraine ikiwemo ya kuunganishwa na ardhi ya Russia eneo la Ukraine la rasi ya Crimea, lakini Marekani pia ambayo ni mwanachama na mdau mkubwa na muhimu zaidi wa NATO ina mtazamo sawa na huo wa washirika wake wa Ulaya kuhusiana na Russia.
Kuhusiana na suala hilo, alipohutubia kikao hicho cha mawaziri wa mambo ya nje wa NATO, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson, alikosoa vikali kile alichokiita siasa shambulizi za Russia nchini Ukraine na katika maeneo mengine ya dunia hususan mashariki mwa Ulaya. Katika jibu lake kwa matamshi hayo ya Tillerson, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa taarifa na kueleza kuwa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika kikao cha Brusels kwamba sera za Moscow ni za kuchochea mivutano, hayakubaliki.
Ukweli ni kwamba Russia haikutarajia serikali ya mpya ya Marekani, ambayo imekuwa kila mara ikitoa kauli za kujenga matumaini ya kuboreshwa uhusiano wa Moscow na Washington, ingechukua msimamo mkali kama huo kuhusiana na Russia. Na hasa ikikumbukwa kuwa Rais Donald Trump wa Marekani ametamka hapo kabla kwamba anataka kuangaliwa upya uhusiano wa Washington na Moscow.
Ukweli ni kuwa kikao cha Brussels, cha mawaziri wa mambo ya nje wa NATO kinaweza kutathminiwa kama sisitizo la kuendelea kukabiliana na Russia na kuchukua hatua zaidi za kijeshi hususan mashariki mwa Ulaya kwa madhumuni ya kuzima kile kinachoelezwa na NATO kama mipango inayohofiwa kutekelezwa na Moscow katika eneo hilo muhimu na hasasi.
Na hasa kwa kuzingatia kuwa wanachama wa Ulaya mashariki wa NATO hususan jamhuri tatu za Baltiki, yaani Estonia, Latvia na Lithuania pamoja na Poland zimetaka hatua kali zaidi zichukuliwe kukabiliana na Russia. Kuhusiana na suala hilo, mbali na NATO kuweka zana za kijeshi katika nchi hizo nne imepeleka pia maelfu ya askari katika ardhi za nchi hizo.
Inavyotarajiwa, katika kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa NATO kitakachofanyika Brussels tarehe 25 ya mwezi ujao wa Mei hatua zaidi zitachukuliwa katika uwanja huo. Kwa hakika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa shirika hilo la kujihami la kijeshi kimefanyika kwa ajili ya maandalizi ya kikao hicho cha wakuu wa nchi wanachama kinachotazamiwa kuhudhuriwa pia kwa mara ya kwanza na Rais Donald Trump wa Marekani.../