Kongamano la kimataifa kwa ajili ya kupambana na ugaidi lafanyika Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27826-kongamano_la_kimataifa_kwa_ajili_ya_kupambana_na_ugaidi_lafanyika_pakistan
Kongamano la pili la kimataifa lililopewa jina la 'Ujumbe wa Uislamu' kwa ajili ya kupambana na ugaidi, kufurutu mipaka na ukatili unaotokana na tofauti, limefanyika nchini Pakistan kwa kuhudhuriwa na maelfu ya maulama wa ndani na nje ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2017 23:44 UTC
  • Kongamano la kimataifa kwa ajili ya kupambana na ugaidi lafanyika Pakistan

Kongamano la pili la kimataifa lililopewa jina la 'Ujumbe wa Uislamu' kwa ajili ya kupambana na ugaidi, kufurutu mipaka na ukatili unaotokana na tofauti, limefanyika nchini Pakistan kwa kuhudhuriwa na maelfu ya maulama wa ndani na nje ya nchi hiyo.

Kongamano hilo lililofanyika mjini Islamabad, mji mkuu wa Pakistan limejadili maudhui mbalimbali ikiwemo namna ya kuondoa tofauti, kufurutu mipaka na ugaidi, kuionyesha dunia kunako Uislamu halisi na kadhalika kupinga chuki dhidi ya dini hiyo ya mbinguni na vitendo vya kigaidi, mauaji na kuwanyang'anya watu haki zao za kimsingi.

Moja ya miripuko ya mabomu inayofanywa na makundi ya Kiwahabi

Mwishoni mwa kongamano hilo, washiriki wametia saini hati ambayo inajumuisha vipengee kadhaa kama vile kuzitaka nchi za Kiislamu kuungana, kufanya juhudi zenye lengo la kuhitimisha vitendo vya kigaidi na kuchupa mipaka katika jamii ya Kiislamu na kupinga vikali mwenendo wa kuuhusishwa Uislamu na ugaidi sambamba na kuhimiza juu ya mazungumzo ya pamoja baina ya madhehebu za Kiislamu na dini nyingine. Pakistan ni kati ya nchi ambazo zimekuwa zikishuhudia mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Waislamu, kiasi cha kuwafanya wailalamikie serikali ya Islamabad kutokana na uzembe wake juu ya suala hilo. Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Baraza la Umoja wa Kiislamu nchini Pakistan alinukuliwa akisema kuwa, baadhi ya mawaziri wa serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nawaz Sharif wanashirikiana na makundi ya kigaidi na ukufurishaji katika kuwaua watu wasio na hatia nchini humo. 

Allameh Raja Nasir Abbas Jafar, akisalimiana na Waislamu wa wenzake nchini Pakistan

Allameh Raja Nasir Abbas Jafar, aliyeyasema hayo mjini Khairpur, mkoa wa Sindh alibainisha kwamba, mahusiano ya baadhi ya mawaziri wa serikali ya Pakistan na makundi ya kigaidi sambamba na kusababisha matatizo makubwa, yamezua pia machafuko nchini humo.