Korea Kaskazini imewatia nguvuni raia 3 wa Marekani
Katika hali ambayo taharuki ingali imetanda katika Peninsula ya Korea, serikali ya Korea Kaskazini imemtia mbaroni raia wa Marekani, na kupelekea idadi ya Wamarekani wanaozuiliwa na serikali ya Pyongyang hadi sasa kufikia watatu.
Ubalozi wa Sweden mjini Pyongyang umethibitisha habari hizo za kukamatwa raia huyo wa Marekani nchini Korea Kaskazini ingawaje haujatoa maelezo zaidi kuhusu sababu za kukamatwa kwake.
Shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini kadhalika limethibitisha habari hizo na kufafanua kuwa, raia huyo wa Marekani aliyetambuliwa kwa jina moja la Kima na ambaye yuko katika miaka ya 50, alikamatwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Pyongyang, alipokuwa akijaribu kuondoka nchini humo kwenda Marekani.
Mbali na raia huyo anayesemekana kuwa Profesa katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Yanbian cha China na ambacho kina tawi mjini Pyongyang; raia mwengine wa Marekani ambaye yuko katika gereza la Korea Kaskazini ni Otto Warmbier aliyehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuiba bango lenye jumbe za propaganda, na Mmarekani mwenye asili ya Korea Kaskazini Kim Dong-chul anayetumikia kifungo cha 10 jela kwa tuhuma za ujasusi.
Haya yanaarifiwa katika hali ambayo, serikali ya Pyongyang imetangaza utayarifu wake wa kukabiliana na hatua yoyote ya kichokozi ya Marekani. Hii ni kufuatia hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kutuma meli zake za kivita katika maji ya Peninsula ya Korea.