Papa akerwa na matumizi ya neno "Mama" kwa bomu la Marekani
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amekosoa vikali hatua ya Marekani ya kulipa bomu lenye nguvu kubwa zaidi la nchi hiyo lisilo la nyuklia jina la "Mama''.
Papa amesema binafsi alikerwa na kusikitishwa mno baada ya kusikia Marekani imetumia neno la heshima la "Mama" kuashiria bomu lake lenye uwezo mkubwa.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesema: "Mama analeta uhai (kwa kujifungua) ilhali bomu hilo linatoa uhai, na linaitwa mama, nini kinaendelea?"
Mwezi uliopita wa Aprili, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, ilitangaza kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa jeshi la nchi hiyo limetumia bomu lake kubwa zaidi lisilo la nyuklia katika viunga vya mji wa Achin kwenye mkoa wa Nangarhar huko Afghanistan.
Bomu hilo la GBU-43B maarufu kwa jina la "Mama wa Mabomu Yote" lina uzito wa tani 11 za mada za milipuko ya TNT na ndilo lenye uharibifu mkubwa zaidi kuliko mabomu yote yasiyo ya nyuklia duniani.
Asasi na shakhsia mbali mbali duniani akiwemo rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai walikosoa kitendo hicho cha Marekani, cha kufanyia majaribio bomu lake hilo katika ardhi ya nchi huru. Karzai alisema kitendo hicho cha Marekani hakina uhusiano wowote na vita dhidi ya ugaidi, lakini ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kujitawala Afghanistan, na kusisitiza kuwa ni jambo lisilokubalika kuifanya nchi hiyo kuwa sehemu ya kufanyia majaribio ya silaha zake mpya na hatari.