Ulimwengu Wachukizwa na Utawala wa Kizayuni katika Siku ya Nakba
Huku dunia ikikaribia kukumbuka mwaka wa 69 wa kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na baada ya hapo kuasisiwa utawala bandia wa Israel, siku ambayo Wapalestina wanaitaja kuwa siku ya Nakba yaani nakama au maafa, walimwengu wanashuhudia wimbi jipya la kimataifa la kuchikizwa na utawala wa Kizayuni na ongezeko la uungaji mkono kwa Wapalestina.
Tarehe 14 Mei mwaka 2017 inasadifiana na mwaka wa 69 wa utawala wa Kizayuni wa Israel kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina maarufu kama SIku ya Nakba. Katika siku kama hii, Wazayuni, kwa himaya ya Uingereza na baada ya miongo kadhaa ya kutekeleza njama, walikalia kwa mabavu na kughusubu ardhi za Palestina zilika.
Baada ya kughusubiwa ardhi za Palestina mnamo Mei 15 1948 Wazayuni walianza oparesheni ya kuwatimua hatua kwa hatua mamia ya maelefu ya Wapalestina kutoka ardhi zao asili na za jadi.
Hivi sasa Wapalestina waliotimuliwa kutoka ardhi zao wameongezeka na kuwa mamilioni na wanaishi katika nchi za kigeni katika hali ngumu na ya kusikitisha sana.
Kwa kuangazia matokeo ya kuanzishwa utawala wa Kizayuni katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina, siku hii hukumbukwa kama siku ya Nakba yaani siku a maafa na majanga kwa jamii ya mwanadamu.
Kwa hakika janga la kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina ni doa na dosari kubwa katika jamii ya walimwengu na mfumo wa kimataifa. Hivi sasa baada ya kupita miaka 69 kadhia ya Palestina haijatatuliwa kwani mamilioni ya wakimbizi Wapalestina bado hawajaweza kutimiza ndoto yao ya kurejea katika ardhi zao za jadi walizopokonywa.
Azimio 194 la Umoja wa Mataifa linasisitiza kuhusu kutatuliwa mgogoro wa wakimbizi Wapalestina lakini tatizo hili bado halijaweza kutafutiwa ufumbuzi na sasa ni changamoto kubwa kwa jamii ya kimataifa. Bila kutatuliwa suala hilo la mamilioni ya wakimbizi Wapalestina hakuna muafaka unaoweza kufikiwa kuhusu kadhia ya Palestina kwani wakimbizi hao wanaishi katika hali ngumu sana katika nchi zinazowapa hifadhi.
Chanzo cha Israel kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina ni matokeo ya njama ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 1897 huko Uswisi. Baada ya dola la kikoloni la Uingereza kuchukua udhibiti wa Palestina na kisha baada ya hapo Tangazo la Balfour mwaka 1917, ulianza utangulizi wa kuundwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina. Mchakato huu uliendelea hadi November 29 mwaka 1947 wakati Umoja wa Mataifa ulipapasisha azimio 181 kuhusu Palestina.
Nchi 23 ikiwemo Marekani, Uingereza na nchi kadhaa za Ulaya zilipiga kura ya kuunga mkono azimio hilo la kunyakuliwa ardhi za Palestina.
Azimio 181 lilipasishwa mwaka mmoja kabla ya kuanza maafa makubwa ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na ni wazi kuwa kulikuwa na njama ya kimataifa ya madola ya kibeberu kuunda utawala wa Kizayuni na bandia wa Israel.
Tokea 14 Mei mwaka 1948, utawala bandia wa Israel ulitangaza rasmi uwepo wake na baada ya hapo Wapalestina daima wamekuwa wakikumbwa na masaibu, maafa, majanga na kuishi kama wakimbizi.
Watetezi wa haki za binadamu duniani wamekuwa wakionyesha kufungamana kwao na Wapalestina na hivi sasa matukio ya kimataifa yanaashiria kuzingatiwa zaidi kadhia ya mgogoro wa Palestina huku waliowengi wakitaka Wapalestina wapewe haki zao.
Jambo hilo linaashiria kufeli utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake hasa Marekani. Katika kujaribu kupotosha kadhia ya Palestina, Marekani na Wazayuni wanatumia mbinu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuchochea fitina Mashariki ya Kati kwa kuibua makundi ya magaidi wakufurishaji.
Lakini katika vikao kadhaa vya kieneo na kimataifa, Wapalestina wamekuwa wakipata uungaji mkono huku kukiwa na harakati kadhaa za kuwaunga mkono kote duniani. Ni wazi kuwa walimwengu wanalalamikia vikali jinai za Utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na wanataka taifa hilo madhulumu lirejeshewe haki zake.
Hii ni katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukipuuza maazimio ya kimataifa na kukiuka mikataba ya kimataifa kuhusu Wapalestina na hayo yote yameweka wazi utambulisho wa Israel kama utawala ghasibu na dhalimu.
Matukio ya kimataifa katika miaka ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa, hata serikali za Ulaya ambazo zimekuwa zikihesabiwa kuwa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni nazo pia zimechoshwa na sera za utawala huo ghasibu. Hivi sasa aghalabu ya nchi nyingi za Ulaya ziko chini ya mashinikizo ya wananchi na zimelazimika kutizama upya sera zao za kuunga mkono Israel na hivi sasa zinaukosoa wazi wazi utawala huo. Hatua hii inaaashiria kubadilika maingiliano ya Ulaya na Utawa wa Kizayuni na kwa msingi huo nchi hizo haizuungi tena bila masharti utawala huo wa kibaguzi kama zilivyokuwa zikifanya huko nyuma.