Ayatullah Araki asisitiza kuimarishwa uhusiano wa nchi za Kiislamu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa, nchi za Shirikisho la Urusi zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla katika kukuza uhusiano wa nchi za Kiislamu na vilevile kuinua kiwango chao cha nafasi ya kisiasa na kiuchumi duniani.
Ayatullah Mohsin Araki amesema hayo pambizoni mwa mkutano wa "Russia na Ulimwengu wa Kiislamu" katika Jamhuri ya Chechnia alipokutana na kufanya mazungumzo na Rustam Minnikhanov, Rais wa Jamhuri ya Tatarstan ya Russia na kueleza kuwa, Iran inaweza kuanzisha ushirikiano wa kielimu na kiutafiti na Vyuo Vikuu vya Jamhuri za Russia.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amemualika pia Rais wa Jamhuri ya Tatarstan kushiriki katika mkutano wa Umoja wa Kiislamu utakaofanyika Disemba mwaka huu hapa mjini Tehran.
Kwa upande wake, Rais Rustam Minnikhanov, wa Jamhuri ya Tatarstan ameitaja Iran kuwa nchi yenye utamaduni mkongwe na kwamba, itikadi ya wananchi wa Iran kwa utamaduni na ada za kidini ndiko kulikolinyanyua kiutamaduni taifa hili.
Ayatullah Mohsin Arakai amekutana na kufanya mazungumzo pia na Mustafa Barghouthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina na kubainisha kwamba, mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kadhia ya Palestina sio mtazamo wa kisiasa bali ni muono na mtazamo ambao chimbuko lake ni itikadi na matukufu ya kidini.
Mkutano wa tatu wa "Russia na Ulimwengu wa Kiislamu" ulifanyika Jumanne ya juzi katika Jamhuri ya Chechnia mada kuu ikiwa ni ushirikiano wa kiuchumi na vita dhidi ya ugaidi.