Putin: Marekani inatumia ugaidi kama wenzo
Huku mivutano kati ya Moscow na Washington ikiwa imepamba moto, Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa, Marekani inawaunga mkono magaidi wa Chechniya huko Kaukazia Kaskazini na kuwatumia magaidi hao kuvuruga usalama na utilivu wa Russia. Rais Putin amesema Idara za Intelijensia za Marekani zimewapa misaada ya kiintelijensia, kisiasa, kifedha na kadhalika magaidi Chechniya licha ya malalamiko na upinzani wa Moscow.
Kwa mtazamo wa Putin, licha ya viongozi wa Marekani kudai kuwa wanaiunga mkono Moscow katika mapambano dhidi ya ugaidi, lakini kivitendo, Washington inawatumia magaidi kuvuruga amani na utulivu ndani ya Russia. Uungaji mkono wa Marekani kwa magaidi wa Kaukazia Kaskazini umefanyika waziwazi na Russia ina ushahidi wa kutosha kuhusiana na suala hilo na baadhi ya ushahidi huo umekabidhiwa kwa viongozi wa Marekani. Rais Putin aliwahi kufichua huko nyuma kwamba, vyombo vya usalama vya Marekan na maafisa wa Idara za Intelijensia ya nchi hiyo wamekuwa wakiwasiliana moja kwa moja na magaidi wa Kaukazia Kaskazini.
Ni wazi kuwa, Russia imekuwa ikikabiliwa na chuki na uhasama wa nchi za Magharibi kwa muda sasa tangu baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti mwaka 1991. Licha ya matarajio ya awali ya Warussia kwa wamagharibi katika muongo wa 1990 wakati wa utawala wa Boris Yeltsin, lakini mienendo isiyo ya kirafiki na ya kiadui ya Marekani, iliwafanya Warussia watambue kwa haraka kwamba, lengo la Magharibi hususan Marekani, ni kuidhoofisha zaidi nchi ya Russia na mwishowe kuigawa. Rais Vladimi Putin wa Russia alitambua mapema jambo hilo na tangu mwanzoni mwa muongo wa 2000 amekuwa akikosoa mienendo na utendaji wa Marekani mkabala wa nchi yake.
Hata katika uwanja wa kupambana na ugaidi ambapo Marekani inadai kuongoza mapambano eti dhidi ya ugaidi duniani, Moscow ilitaraji kupata uungaji mkono na ushirikiano kutoka nchi za Magharibi, lakini badala ya kuungwa mkono, imeshuhudia idara za intelijensia za Marekani zikiwaunga mkono kwa hali na mali magaidi.
Chuki za Magharibi dhidi ya Russia haziishii katika suala la ugaidi, bali Marekani imekuwa ikiwachochea wananchi wa Russia na kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali ya Moscow. Hatua zote hizo zinatekelezwa na Marekani chini ya anwani ya "Mapinduzi ya Rangi". Viongozi wa ngazi ya juu wa Russia wanaamini kuwa, juhudi zinazofanywa eti kwa lengo la kupeleka nje demokrasia na mapinduzi ya rangi ni miongoni mwa sababu kuu za kuweko machafuko na ukosefu wa amani katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa utaratibu huo, Moscow si tu kwamba imekuwa ikikosoa sera hizo za mapinduzi ya rangi duniani, bali kabla ya hapo ilikuwa ikihofia kutokea mapinduzi laini katika nchi za Urusi ya zamani ikiwemo Russia yenyewe.
Kuhusiana na suala hilo, Alex Poshkov, Mkuu wa Kamisheni ya Masuala ya Kimataifa katika Bunge la Russia (Duma) amesema kuwa, Magharibi imeandaa mkakati wa aina tatu ili kutekeleza mapinduzi ya rangi huko Russia. Kwa mtazamo wa Poshkov, mpango wa kwanza ni kuibua maandamano makubwa mjini Moscow kama yale yaliyowahi kushuhudiwa katika Medani ya Uhuru mjini Kiev kwa kutumia wapinzani wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi. Mpango wa pili ni kumfikisha madarakani nchini Russia kiongozi na rais anayeiunga mkono Marekani na wa tatu ni kutekeleza vikwazo vya kiuchumi vya Magharibi na Marekani dhidi ya Russia. Viongozi wa Magharibi wanataraji kuwa, kupitia njia hizo, watafanikiwa kuchochea malalamiko na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali ya Moscow na hivyo kuandaa mazingira ya kumuondoa madarakani Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo.
Kwa ujumla ni kuwa, lengo kuu la Marekani ni kuidhoofisha Russia ama kupitia njia ya kueneza machafuko au kuwaunga mkono magaidi ili kutekeleza hujuma na vitendo haribifu dhidi ya Moscow.