Hali ya Palestina katika Siku ya Kimataifa ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30850-hali_ya_palestina_katika_siku_ya_kimataifa_ya_quds
Leo tarehe 23 Juni inayosadifiana na Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ambayo ilitangazwa na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhullah Khomeini kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2017 03:21 UTC
  • Hali ya Palestina katika Siku ya Kimataifa ya Quds

Leo tarehe 23 Juni inayosadifiana na Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ambayo ilitangazwa na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhullah Khomeini kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds.

Hapana shaka kuwa, Palestina na Wapalestina ndio kaumu iliyodhulumiwa zaidi katika historia kwa sababu utawala bandia wa Israel umevamia na kutwaa kwa mabavu ardhi na nchi yao, ukawafanya wakimbizi ndani ya nje ya Palestina, ukawasulubu kwa aina mbalimbali za mateso, kuwaua, kubomoa nyumba na maeneo yao matakatifu na kuweka mzingiro wa pande zote kwa watu wanaoendelea kufa taratibu wa Ukanda wa Gaza. Sambamba na hayo utawala huo bandia unakusanya Mayahudi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia ya kuwajengea vitongoji vya walowezi katika ardhi iliyoghusubiwa huko Palestina. Jinai kama hizo kwa pamoja hazijawahi kufanywa au kushuhudiwa zikifanywa na utawala mmoja dhidi wakazi na watu wa kaumu moja katika historia. Ni kwa kutulia maanani jinai hizo zote ndipo mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Ruhullah Khomeini akaitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimatifa ya Quds kwa shabaha ya kukumbusha dhulma kubwa inayofanywa dhidi ya Wapalestina na kudhihirisha sehemu ya ukatili na unyama huo.

Imam Khomeini

Hii leo Waislamu na wapenda haki kote duniani wanashiriki katika maandamano na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds huku suala la Palestina likiwa limeondolewa katika ajenda muhimu ya masuala ya ulimwengu wa Kiislamu au kuwekwa kandokando, na wakati huo huo Israel ikizidisha ukatili na mauaji dhidi ya Wapalestina.  

Palestina katika miaka ya huko nyuma ilikuwa kadhia kuu na kipaumbele cha kwanza cha watawala wa nchi za Kiarabu hususan wale wanaodai kuwa vinara wa ulimwengu wa Kiarabu. Hata hivyo hii leo ripoti na ushahidi vinaonesha kuwa, nchi hizo hizo za Kiarabu zinaimarisha zaidi uhusiano na mawasiliano yao na dola haramu la Israel. Marwan Abdul Adil ambaye ni afisa wa Harakati ya Wananchi kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina amesema katika mkutano ulioitishwa na Ofisi ya Utamaduni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Beiruti nchini Lebanon kuwa: Kadhia ya Palestina imepoteza nafasi na umuhimu wake katika eneo la Mashariki ya Kati. Kwa upande wake, mwakilishi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina nchini Lebanon, Abu Imad al Rifai' amesema katika mkutano huo kwamba: Hii leo Palestina na watu wake hawakabiliwe na vitisho vya utawala haramu wa Israel pekee bali pia vitisho vya baadhi ya nchi za Kiarabu.

Mfalme Salman wa Saudia akiwa pamoja na Donald Trump

Ni katika mazingira hayo ndipo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akapuuza tena azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika siku za kabla kidogo ya madhimisho ya siku ya leo na kupasisha mradi wa ujenzi wa zaidi ya nyumba elfu saba na vitongoji vipya vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Hayo yamefanyika sambamba na mauaji ya vijana wa Kipalestina.

Suala jingine chungu kuhusu kadhia ya Palestina ni kwamba, wakati nchi za Kiarabu zikiliweka kando suala la Wapalestina na haki zao, waungaji mkono wa Israel hususan Marekani wamezidisha uungaji mkono na misaada yao kwa Wazayuni maghasibu. Katika mkondo huo mjumbe wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jason Greenblatt na vilevile mkwe wake, Jared Kushner walitumwa huko Israel siku chache kabla ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kufanya mazungumzo na Waziri wake Mkuu, Benjamin Netanyahu. Wajumbe hao wa Trump wamesisitiza tena kuwa, Marekani itaendelea kuiunga mkono na kuisaidia Israel kwa hali na mali.

Ujumbe wa Trump ukiwa pamoja na Netanyahu

Kwa kutilia maanani hayo yote, maandamano makubwa yanayofanywa na Waislamu na wapenda haki katika maeneo mbalimbali ya dunia hii leo katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani yatathibitisha tena kwamba, japokuwa kadhia ya Palestina imetupiliwa mbali na kupuuza na watawala na viongozi tegemezi wa nchi za Kiarabu na zile zinazojiita za Kiislamu, lakini Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu kitaendelea kuwa hai katika nyoyo, fikra na akili za Waislamu wote Waarabu na wasio Waarabu, na wapigania haki na uadilifu kote duniani.