Mafanikio ya Wapalestina katika uga wa kimataifa
-
Bendera ya Palestina ikipepea katika ofisi za UNESCO mjini Paris Ufaransa
Hatua ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ya kuuweka mji wa al Khalil na Haram ya Nabii Ibrahim AS katika orodha ya turathi za dunia zilizoko kwenye hatari ya kuangamia, inaonesha kuendelea kupata Wapalesstina ushindi wa kimataifa wa kidiplomasia.
Hatua hiyo ya UNESCO imeakisiwa kwa wingi duniani na hilo linaonesha namna suala la Palestina lilivyo hai na linavyopewa umuhimu mkubwa na walimwengu.
Juzi Ijumaa, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliutaja mji wa al Khalil katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Haram ya Nabii Ibrahim AS kuwa ni katika turathi za kihistoria za dunia ambazo zinakabiliwa na hatari kubwa ya kuangamizwa.
Hatua hiyo ya UNESCO imechukuliwa licha ya kuweko upinzani mkali kutoka kwa Marekani, Israel na Canada na licha ya madola hayo kuweka mashinikizo makubwa mno dhidi ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa. Kuingizwa maeneo hayo mawili muhimu ya Palestina katika orodha ya turathi za dunia ni pigo jingine kwa utawala wa Kizayuni ambao unafanya njama za kila namna za kuisahaulisha kadhia ya Palestina. Mji mtakatifu wa Bayatul Muqaddas nao uliingizwa kwenye orodha ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ya turathi za kihistoria na huo ukawa ushindi mwingine mkubwa wa kimataifa kwa taifa linalokandamizwa la Palestina. Mwakilishi wa utawala wa Kizayuni amewakasirisha sana wawakilishi wa nchi nyingine duniani kutokana na hamaki na matamshi yake ya kejeli aliyoyatoa katika kikao kilichopasisha kuwa mji wa al Khalil na Haram ya Nabii Ibrahim AS ni katika turathi za kihistoria.
Baada ya kupasishwa muswada huo, mwakilishi wa Israel katika kikao hicho alifanya ukaidi wa kutosikiliza amri ya mwenyekiti wa kikao. Mwakilishi huyo wa Israel alifanya fujo na kuropoka maneno ya kipuuzi ili kuvuruga kikao hicho, kabla ya kuondoka kwa jeuri kikaoni hapo hata kabla ya kumalizika. Hata hivyo yote hayo hayakuwazuia wajumbe wengine kuchukua hatua inayofaa ya kuutangaza mji wa al Khalil na Haram ya Nabii Ibrahim AS kuwa ni katika turathi za kihistoria zilizoko kwenye hatari ya kuangamizwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika kikao chake kimoja cha kujadili hali hiyio, gazeti la al Safir la nchini Lebanon limeashiria maazimio ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuhusiani na Palestina na namna shirika hilo linavyosisitiza mara kwa mara kuwa maeneo matakatifu huko Palestina ni ya Wapalestina, na Israel haina haki yoyote ya kutia mkono wake kwenye masuala ya maeneo hayo. Limeandika: UNESCO imetoa pigo jingine kubwa kwa utawala wa Kizayuni, licha ya njama kubwa zinazofanywa na Israel dhidi ya shirika hilo.
Hatua ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ya kuipa Palestina uanachama kwenye shirika hilo na hivyo kuruhusu bendera ya Palestina ipeperushwe kwenye makao makuu ya shirika hilo mjini Paris Ufaransa tangu mwezi Disemba 2011 lilikuwa ni tangazo la wazi la uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa haki za Wapalestina.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa mara zote ukifanya njama za kila namna za kutaka kulisahaulisha kabisa suala la Palestina duniani. Israel inafanya njama za kila namna, ikiwa ni pamoja na kubadilisha majina ya Kiarabu ya maeneo ya Palestina na kuyapachika majina ya Kiyahudi, kuwalazimisha Wapalestina kuyahama makazi yao na kuwapelekea huo walowezi wa Kizayuni, kuvunja athari zote za Wapalestina ikiwemo misikiti na maeneo matukufu ya Wapalestina. Kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa namna ambayo inayakata vipande vipande maeneo ya Palestina sambamba na kujenga ukuta wa kibaguzi ulioyatenganisha vibaya maeneo ya Wapaelstina hao. Yote hayo yanafanywa na Israel ili kufuta kabisa kitu kinachoitwa ardhi za Palestina katika uso wa dunia. Hata hivyo kadiri siku zinavyopita ndivyo mashirika mbalimbali ya kimataifa yanavyochukua hatua za kuibakisha hai kadhia ya Palestina. Si hayo tu, uungaji mkono wa walimwengu kwa taifa la Palestina nao unazidi kuwa mkubwa siku hadi siku na hilo ni pigo jingine kubwa kwa utawala pandikizi wa Kizayuni na ni ushindi usio na kifani kwa taifa madhlumu la Palestina.