Viongozi wa Kiislamu Ulaya waanza safari ya kulaani ugaidi
Makumi ya viongozi wa kidini na maimamu wa Swala za jamaa barani Ulaya wameanza safari ya kutembelea nchi kadhaa za bara hilo wakitokea mtaa mashuhuri wa Champs-Elysees mjini Paris. Viongozi hao wa kidini watatembelea maeneo yaliyokumbwa na mashambulizi ya kigaidi katika miezi ya hivi karibuni.
Maimamu wa Swala za jamaa kutoka nchi kama Ufaransa, Ubelgiji na Uingereza na wawakilishji wa madhehebu nyingine za kidini wameanza safari hiyo ya kuwakumbuka wahanga wa mashambulizi ya kigaidi na kulaani ukatili kutokea eneo lililoshuhudia tukio la kuuawa afisa mmoja wa polisi kwa kupigwa risasi mjini Paris mwezi Aprili mwaka huu.
Watayarishaji wa safari hiyo wanasema kuwa, msafara huo unaelekea Berlin nchini Ujerumani ambako utakutana na Kansela wa nchi hiyo, Angela Merkel. Viongozi hao wa kidini pia watatembelea miji ya Brussels nchini Ubelgiji na Nice huko kusini mwa Ufaransa na watarejea Paris tarehe 14 Julai, siku ya kumbukumu ya shambulizi ya kigaidi la Daesh katika mji wa Nice lililofanyika kwa kutumia lori.

Kundi la kigaidi la Daesh lilikiri kwamba, ndilo lililofanya shambulizi hilo wakati raia wa Ufaransa walipokuwa katika sherehe ya siku ya kitaifa ya Bastille katika mji wa Nice na kuua watu wasiopungua 86. Kundi hilo pia lilihusika na shambulizi lililolenga soko la Krismasi mjini Berlin Disemba mwaka jana na kuua watu 12.
Hassan Shalfomi ambaye ni miongoni mwa watayarishaji wa safari hiyo anasema, moja kati ya malengo yake ni kutangazia dunia kwamba Uislamu na mafundisho yake vinapinga ugaidi.