Matokeo ya mazungumzo ya Trump na Putin mjini Hamburg Ujerumaini
Baada ya kupita miezi mingi ya malalamiko ya Wamarekani kwa Russia wanaodai kuwa Moscow inaingilia masuala ya ndani ya nchi yao, hatimaye marais wawili wa nchi hizo mbili wamekutana pambizoni mwa kikao cha viongozi wa G20 mjini Hamburg, Ujerumani. Hayo yalikuwa ni mazungumzo ya kwanza ya marais hao wawili tangu Donald Trump atangazwe kuwa rais wa Marekani.
Kati ya mazungumzo ya pande mbili na pande kadhaa yaliyofanyika wakati wa kikao cha viongozi wa kundi la G20 mjini Hamburg Ujerumani, mazungumzo kati ya Vladimir Putin na Donald Trump, marais wa Russia na Marekani ndiyo yaliyopewa umuhimu na kuakisiwa kwa wingi zaidi duniani. Kwa mujibu wa viongozi wa nchi hizo mbili, Moscow na Washington hivi sasa zina uhusiano wa chini mno ikilinganishwa na kipindi chote hiki cha baada ya vita baridi. Russia imewekewa vikwazo na Marekani kwa sababu kadhaa yakiwemo madai ya kuingilia Moscow masuala ya ndani ya Ukraine na vile vile tuhuma kuwa Russia iliingilia na kuathiri matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchini Marekani. Katika upande wa pili, Russia nayo imechukua hatua kama hizo za kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Marekani kama ambavyo Moscow imepata mafanikio makubwa dhidi ya madola ya Magharibi yanayoongozwa na Marekani katika maeneo nyeti kama Ulaya Mashariki, Asia Magharibi na Afrika Kaskazini. Mafanikio hayo makubwa iliyopata Moscow yamepelekea kupata nguvu mno hisia zilizo dhidi ya Russia ndani ya Marekani. Hivi sasa timu ya uchaguzi ya Donald Trump inatuhumiwa ilikuwa na uhusiano wa siri na usio wa kawaida na Russia wakati wa kampeni za uchaguzi wa Marekani.
Pamoja na hayo, mazungumzo ya Trump na Putin na miafaka iliyofikiwa baada ya mazungumzo hayo huko Hamburg Ujerumani, yanaonesha kuwa, kwa uchache viongozi wa Ikulu ya Marekani White House hawana hisia kali sana dhidi ya Russia ikilinganishwa na duru nyinginezo nchini humo. Inasemekana kuwa, wakati wa mazungumzo hayo, Trump alikubaliana na maelezo ya Putin kuhusu kutojihusisha kivyovyote vile Russia na uchaguzi wa Marekani, suala ambalo haliwezi kamwe kukubaliwa na mrengo wa maadui wa Russia ndani ya Marekani. Viongozi hao wawili wa Marekani na Russia walikubaliana pia kusimamisha vita katika baadhi ya maeneo nchini Syria. Tabán Rex Tillerson, waziri wa mambo ya nje wa Marekani alidai kuwa Washington haiafiki watu wa Rais Bashar al Assad kuwa na nafasi yoyote katika muundo ujao wa uongozi wa Syria. Matamshi hayo ya Tillerson yanahesabiwa na wachambuzi wa mambo kuwa yamelenga kupunguza hisia kali za mrengo wa maadui wa Russia ndani ya Marekani kutokana na mazungumzo hayo ya Trump na Putin. Katika upande mwingine, mara kwa mara Russia imekuwa ikitangaza wazi uungaji mkono wake kwa Rais Bashar al Assad wa Syria kama ambavyo Moscow imekuwa ikisisitiza sana kwamba, wenye haki ya kuamua mustakbali wa Syria na viongozi wa baadaye wa nchi hiyo, ni Wasyria wenyewe, si mtu mwingine yeyote. Inatabiriwa kuwa mashinikizo dhidi ya rais wa Marekani, Donald Trump yataongezeka hivi sasa baada ya kukutana kwake na Rais Vladimir Putin wa Russia huko Hamburg, Ujerumani.
Fareed Zakaria, ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa televisheni ya CNN ya Marekani. Amesema, mazungumzo ya Trump na Putin yanatia wasiwasi mkubwa. Amesema, tatizo alilo nalo Trump ni kuwa hajui kabisa kufanya mambo kiistratijia. Tunashindwa kujua ni vipi huyu Trump ataweza kusimama kukabiliana na Putin kwani hadi hivi sasa hatujamuona na mkakati wala ratiba yoyote ile, na wakati wowote anaweza kuropoka jambo lolote lile.
Alaakullihaal, inavyoonekana ni kuwa, licha ya Donald Trump kuropoka mara kwa mara na kuchukua hatua hizi na zile za pupa, lakini Wamarekani hawana njia za kutosha za kuifanya nchi yao iwe dola pekee kubwa duniani. Mlolongo mrefu wa madola mbalimbali yanayozidi kudhihiri siku hadi siku na kutafuta nafasi katika milingano ya matukio duniani, ni mpinzani mkubwa wa Marekani katika ndoto zake za kujifanya dola pekee lenye nguvu ulimwenguni. Kudhihiri Donald Trump hivi sasa pia kuna hatari ya kuharakisha kupungua ushawishi wa Marekani kimataifa hasa kutokana na misimamo mikali inayochukuliwa na mirengo inayomuunga mkono Trump.