Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Uingereza wazidi kulalamikiwa kimataifa
Taasisi za kutetea haki za binadamu nchini Uingereza zimekosoa kuendelea mchakato wa kuiuzia silaha Saudi Arabia ili izitumie katika mashambulizi yake dhidi ya raia wa Yemen wasio na hatia.
Baada ya Mahakama Kuu ya Uingereza kupinga ombi la kusimamisha uuzaji wa silaha za nchi hiyo kwa Saudia na waitifaki wake na kisha mahakama hiyo kuitaja hatua hiyo kuwa si kinyume cha sheria, taasisi za kiraia, za kutetea haki za binadamu na wanarakati wa kisiasa wameonyesha radiamali yao kwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Uingereza na kuutaja kuwa ni sawa na kushiriki katika kukiuka sheria za haki za binadamu na kutekeleza mauaji dhidi ya raia wa Yemen.
Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International pia limekosoa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Uingereza wa kuruhusu kuendelea kuuziwa silaha Saudia na kuutaja kuwa ni wenye kukatisha tamaa na unaokiuka maazimio ya Uingereza na hati za makubaliano ya kimataifa.
Maazimio ya kimataifa yanapiga marufuku kuunda, kuuza na kutumiwa mabomu ya vishada huku nchi nyingi ikiwemo Uingereza zikiwa zimesaini maazimio hayo, hata hivyo viongozi wa nchi hiyo wametangaza wazi katika radiamali yao kwa malalamiko na upinzani uliojitokeza dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kwamba huko nyuma walishaiuzia Saudi mabomu hayo. Ripoti ya Shirika la Kupambana na Biashara ya Silaha nchini Ungereza inaonyesha kuwa serikali ya London imeiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 4 tangu kuanza mashambulizi ya Saudia huko Yemen.