Mashia wa Pakistan wailaumu serikali kwa kushindwa kudhibiti ugaidi
Kiongozi wa Waislamu wa Shia wa Pakistan ambaye pia ni mkuu wa harakati ya Mwamko wa Kiislamu nchini humo amesema kuwa ugaidi ni adui wa ubinaadamu na kamwe hauna mahusiano yoyote na dini.
Allamah Allama Sajid Naqvi sambamba na kulaani vitendo vya ugaidi vya hivi karibuni katika jimbo la Balochistan nchini humo amesema kuwa, serikali ya Nawaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan imeshindwa kudhamini usalama kwa raia na kukabiliana na mashambulizi ya makundi ya kigaidi na badala yake imekuwa ikisalia kimya kuhusiana na mashambulizi hayo.
Aidha Allama Sajid Naqvi ameionya serikali ya Islamabad kwamba ikiwa haitoweza kuzuia mashambulizi ya makundi ya ukufurishaji na kigaidi, basi nchi hiyo itakabiliwa na mgogoro mkubwa sana. Ameongeza kuwa, raia wa Pakistan hawawezi kuendelea kunyamanzia kimya mauaji na jinai zinazofanywa na magaidi kuwalenga Waislamu wa Kishia na kupuzwa suala hilo na kwamba ikiwa mauaji dhidi ya Waislamu hao hayatosimamishwa, basi kutaitishwa maandamano ya nchi nzima. Shambulizi la kigaidi la siku tatu zilizopita dhidi ya Waislamu wa Shia wa mji wa Mastung wa jimbo la Balochistan nchini Pakistan lilipelekea kwa akali watu wanne kuuawa.
Mwezi mmoja uliopita kulijiri miripuko miwili ya kigaidi katika eneo la Waislamu wa Shia la Parachinar, kaskazini maghribi mwa Pakistan na kusababisha zaidi ya watu 150 kuuawa shahidi. Kama kawaida viongozi wa serikali, wamekuwa wakisema kuwa makundi ya Jama'at Ahrara, Sepah Sahabah na Lashgaq Jahangui, ndiyo yanayohusika na hujuma hizo.