Russia yalaani hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo vipya Iran
Mkuu wa Idara ya Kuzuia na Kudhibiti Silaha iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Mikhail Ulyanov amelaani hatua ya kiuhasama ya Marekani katika kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vipya na kusema kuwa, vikwazo hivyo havijazingatia sheria zozote zile.
Jumanne iliyopita Wizara ya Hazina ya Marekani iliwawekea vikwazo watu na mashirika 18 ya Iran na ya kigeni kwa madai tofauti yakiwemo ya kuhusika na mipango ya makombora ya balestiki ya taifa hili. Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya asasi na shakhsia tofauti wa Iran vimejiri katika hali ambayo Rais Donald Trump alitangaza na kukiri kwa mara ya pili siku ya Jumatatu kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Kufuatia hatua hizo kinzani za Marekani, Mikhail Ulyanov amesema kuwa vikwazo vipya dhidi ya Iran vitavuruga tu makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1. Naye kwa upande wake, Sergei Ryabkov Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amekosoa vikali hatua ya serikali ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Tehran na kuitaja kuwa isiyo ya kisheria. Inafaa kuashiria kuwa, tangu alipoingia madarakani, Rais Donald Trump amekuwa akifuata siasa za uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Marekani inadai kuwa, majaribio ya makombora ya Iran yako kinyume na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba makombora hayo eti yanaweza kubeba vichwa vya nyuklia, katika hali ambayo hata Umoja wa Ulaya umekiri kuwa hadi sasa Tehran haijakiuka mapatano ya nyuklia ya JCPOA.