Russia: Makubaliano ya JCPOA yamefichua jinsi Marekani inavyokiuka sheria za kimataifa
(last modified Sat, 22 Jul 2017 16:50:28 GMT )
Jul 22, 2017 16:50 UTC
  • Russia: Makubaliano ya JCPOA yamefichua jinsi Marekani inavyokiuka sheria za kimataifa

Mkuu wa Kituo cha Stratijia za Kisiasa nchini Russia, Sergei Mikheev amesema kuwa, kitendo cha Marekani kukiuka makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA, kimeidhihirisha nchini hiyo kwamba ni mkiukaji mkubwa wa sheria na mikataba ya kimataifa duniani.

Mikheev ameyasema hayo katika mahojino na Shirika la Habari la IRNA kando na kikao cha Kamisheni ya Uratibu wa Utekelezwaji wa makubaliano ya JCPOA mjini Vienna, Austria na kuongeza kuwa, kundi la 5+1 na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilitiliana saini makubaliano hayo ya kimataifa kwa ajili ya kuhitimisha kikamilifu mgogoro wa nyuklia, lakini Marekani imeyakiuka. 

Rais Donald Trump wa Marekani mkiukaji wa makubaliano hayo

Sergei Mikheev ameendelea kusema kuwa, Washington inavunja makubaliano hayo katika hali ambayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa azimio likizitaka pande zilizoyatia saini kuheshimu mkataba huo. Mkuu wa Kituo cha Stratijia za Kisiasa nchini Russia amesema kuwa, hatua mpya ya Marekani ya kukiuka waziwazi makubaliano ya JCPOA, ni kuwawekea vikwazo watu na mashirika 18 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya Tehran kufungamana vilivyo na makubaliano hayo. Marekani ilichukua hatua hiyo inayokiuka sheria za kimataifa dhidi ya Iran kwa kisingizio cha makombora na matukio yanayojiri katika eneo la Mashariki ya Kati.

Makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA siku yalipofikiwa

Mikheev amesisitiza kuwa, Marekani haina haki ya kuchunguza upya makubaliano hayo yaliyokwishatiwa saini na kwamba, licha ya Washington kutaka kufanyike mazungumzo upya kuhusiana na kadhia hiyo, hakutakuwa na mazungumzo hayo na badala yake pande husika zinatakiwa kuheshimu na kuyatekeleza kikiamilifu. Kikao cha Kamisheni ya Uratibu wa Utekelezwaji wa Makubaliano ya JCPOA mjini Vienna, Austria kilichofanyika Ijumaa ya jana mjini Vienna kilimalizika kwa kutolewa tangazo la kuikosoa Marekani kutokana na ukiukaji wa makubaliano hayo.