Kuachiliwa huru kiongozi wa kigaidi nchini Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i3214-kuachiliwa_huru_kiongozi_wa_kigaidi_nchini_pakistan
Katika hali ambayo wananchi wa Pakistan walikuwa wakisubiria kuona vyombo vya mahakama vya nchi hiyo vikiwachukulia hatua kali wahusika wa vitendo vya kigaidi, ndio kwanza vimemuachilia huru kiongozi wa kundi la ukufurishaji na la kigaidi la 'Sepah Sahabah' kutoka jela.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 16, 2016 22:21 UTC
  • Kuachiliwa huru kiongozi wa kigaidi nchini Pakistan

Katika hali ambayo wananchi wa Pakistan walikuwa wakisubiria kuona vyombo vya mahakama vya nchi hiyo vikiwachukulia hatua kali wahusika wa vitendo vya kigaidi, ndio kwanza vimemuachilia huru kiongozi wa kundi la ukufurishaji na la kigaidi la 'Sepah Sahabah' kutoka jela.

Mahkama ya kupambana na ugaidi nchini Pakistan imemuachilia huru kwa dhamana Aurangzeb Farooqi, kiongozi wa kundi hilo la Sepah Sahabah maarufu kwa jina la 'Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa' baada ya kukaa miezi tisa katika jela ya Adyala katika jimbo la Punjab nchini humo. Aurangzeb Farooqi alitiwa mbaroni tarehe sita mwezi Juni mwaka jana, baada ya kutoa matamshi ya fitina na kuibua tofauti baina ya Waislamu katika eneo la Taxila jimboni Punjab. Hatua hiyo imechukuliwa katika hali ambayo jamii ya Pakistan ilikuwa ikitaraji kuona mahakama ya nchi hiyo ikichukua hatua kali kuhusiana na faili la Farooqi kutokana na kuhusika kwake na vitendo vya kigaidi. hata hivyo mahakama hiyo bila ya kuheshimu matakwa ya jamii ya Wapakistan imemuachilia huru kwa dhamana ya watu wawili na kupokea kiasi cha Rupia 2000. Shakhsia huyo amehuhusika na mauaji ya raia wa nchi hiyo hususan Waislamu wa Kishia, huku mikono yake ikitapakaa damu za Wapakistan. Baada ya kutiwa mbaroni Aurangzeb Farooqi, waungaji mkono wa makundi ya kigaidi hususan Sepah Sahaba, walifanya maandamano katika miji ya Rawalpindi na Islamabad kuishinikiza serikali ya nchi hiyo imuachilie huru. Mwaka 2000, serikali ya Islamabad ilizipiga marufuku harakati za kigaidi za kundi hilo. Hata hivyo kundi hilo lilieneleza harakati zake baada ya kubadili jina na kujiita Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa. Itafahamika kuwa, kundi la kigaidi na kitakfiri la Sepah Sahabah, kwa kushirikiana na makundi mengine ya kitakfiri kama vile 'Lashgar Jahangui, limehusika mara kadhaa katika mashambulizi ya kigaidi katika maeneo tofauti ya Pakistan, ukiwemo ulipuaji na utegaji mabomu kando ya barabara na pia kuwaua Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo baada ya kupasishwa pendekezo la kukabiliana na ugaidi nchini Pakistan, raia wa taifa hilo walikuwa wakisubiri kuona serikali ikichua hatua za kivitendo katika uwanja huo bila ya upendeleo. Hatua ya serikali ya Nawaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan ya kupiga marufuku hukumu ya adhabu ya kifo kwa wahusika wa vitendo vya kigaidi na badala yake kufuatiliwa kesi hizo katika mahakama za kijeshi, ilikuwa ikijaribu kuonyesha kuwa serikali yake imeazimia kwa dhati kukabiliana na tatizo hilo la ugaidi sanjari na kuimarisha usalama nchini. Hii ni kwa kuwa shambulio la kigaidi la mwezi Disemba mwaka 2014 dhidi ya chuo cha kijeshi mjini Peshawar,lililichafulia jina jeshi la Pakistan. Katika shambulizi hilo, watu 140 wengi wao wakiwa ni wanafunzi waliuawa. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana weledi wa mambo nchini Pakistan wakaamini kuwa, mienendo na utendaji wa vyombo vya sheria nchini humo, unaonyesha wazi kuwa vyombo hivyo havina uwezo au havitaki kukabiliana na wimbi la makundi ya kigaidi na kitakfiri ambayo ni changamoto kubwa kwa usalama na amani ya nchi hiyo.