Watu 120 wafariki dunia baada ya kusombwa na mafuriko India
Zaidi ya watu 120 wanaripotiwa kufariki dunia nchini India kufuatia janga la mafuriko yaliyotokea magharibi mwa nchi hiyo.
Deepak Ghai, afisa wa Mamlaka ya Kukabiliana na Majanga nchini humo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo yameua watu 120 katika jimbo la Gujarat, magharibi mwa nchi, mbali na kusababisha hasara kubwa ya kusombwa nyumba, mashamba na hata barabara.
Amesema kufikia sasa watu zaidi ya 300 wamepoteza maisha kutokana na janga hilo la kimaumbile katika majimbo ya mashariki na magharibi mwa nchi.
Afisa huyo wa Mamlaka ya Kupambana na Majanga nchini India ameongeza kuwa, zaidi ya familia milioni moja zimeathiriwa na mafuriko hayo katika jimbo la Gujarat baada ya nyumba zao kusombwa na maji, huku makumi ya maelfu ya wakulima wa pamba wakipata hasara kubwa kutokana na kuharibiwa kwa mashamba yao.
Agosti mwaka jana, zaidi ya watu 300 walifariki dunia nchini India kutokana na mafuriko yaliyotokea mashariki na katikati mwa nchi hiyo, hususan katika majimbo ya Madhya Pradesh, Bihar, Uttar Pradesh, Rajasthan na Uttarakhand.
India ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na mafuriko kila mwaka na mamia ya watu hupoteza maisha kutokana na janga hilo la kimaumbile.