Waziri Mkuu wa Pakistan ajiuzulu kufuatia uamuzi wa mahakama
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32386-waziri_mkuu_wa_pakistan_ajiuzulu_kufuatia_uamuzi_wa_mahakama
Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif amejiuzulu wadhifa wake baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kumuengua madarakani kutokana na kashfa ya ufisadi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2017 09:41 UTC
  • Waziri Mkuu wa Pakistan ajiuzulu kufuatia uamuzi wa mahakama

Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif amejiuzulu wadhifa wake baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kumuengua madarakani kutokana na kashfa ya ufisadi.

Akisoma hukumu dhidi yake hii leo, Jaji Ejaz Afzal Khan wa mahakama hiyo amesema Nawaz Sharif amevuliwa ubunge na kwa msingi huo amepoteza wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu wa nchi hiyo.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Pakistan umetolewa baada ya kubainika kuwa, Sharif pamoja na familia yake walikuwa miongoni mwa shakhsia walioficha fedha za umma nje ya nchi kwa maslahi yao binafsi.

Ufichuzi huo uliwekwa hadharani kwa mara ya kwanza na nyaraka za siri zilizofichuka hivi karibuni zijulikanazo kama 'Nyaraka za Panama'.

Nyaraka za Panama

Majaji watano wa Mahakama ya Juu katika mju mkuu Islamabad wamesema baada ya kusikiliza kwa makini na kuangalia ushahidi uliokuwa mbele yao, wamebaini kuwa ni kweli Sharif alihusika na hivyo amekosa uaminifu kwa wananchi wa taifa hilo.

Mbali na Waziri Mkuu, Mahakama ya Juu ya Pakistan pia imetengeua uteuzi wa Ishaq Dar, Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, ambaye alikuwa mpambe wa karibu wa Nawaz Sharif.