Vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu vyaongezeka nchini Ujerumani
Gazeti moja la nchini Ujerumani limeripoti kuwa, hujuma na mashambulio dhidi ya Waislamu yameongezeka mno katika nchi hiyo ya bara Ulaya katika mwaka huu wa 2017.
Gazeti la Die Welt liliandika katika toleo lake la jana Ijumaa kwamba, viongozi wa nchi hiyo wanasema kuanzia mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu, watu 16 wamejeruhiwa nchini humo kutokana na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo ni kuwa, katika kesi na mikasa yote hiyo, watekelezaji wa hujuma na mashambulio hayo ni watu wenye misimamo ya kufurutu ada wa mrengo wa kulia nchini humo ambapo katika matukio hayo yote ni mtu mmoja tu ametiwa mbaroni hadi sasa.
Polisi ya Ujerumani nayo inasema kuwa, katika kipindi cha miezi mitatu ya pili ya mwaka huu yaani kuanzia Aprili hadi Juni kumesajliiwa kesi 192 dhidi ya Waislamu.
Gazeti la Die Welt linaandika kuwa, hujuma na uhalifu unaofanywa dhidi ya Waislamu ni ishara ya kutangaza chuki dhidi ya wafuasi wa dini hiyo ambapo kumekuwa kukitumiwa vitu kama barua za vitisho au kuvamiwa na kushambuliwa wanawake wa Kiislamu wanaovaa vazi la hijabu.
Nchini Ujerumani kuna Waislamu takribani milioni nne na nusu ambao akthari yao wana asili ya Uturuki.
Licha ya vitendo vya chuki na hujuma dhidi ya Waislamu, Uislamu ndio dini inayokuwa kwa kasi zaidi barani Ulaya na watu wengi wamekuwa wakivutiwa na mafundisho ya dini hiyo ya amani licha ya kuweko njama za kila upande za kuchafua sura na sura ya dini hiyo.