Watu milioni 24 waathiriwa na mafuriko Asia ya Kusini
Watu zaidi ya milioni 24 wameathiriwa na mafuriko makubwa kuwahi kulikumba eneo la Asia ya Kusini katika miongo kadhaa iliyopita, huku maeneo mengi ya ardhi yakiwa yameghiriki majini. Hayo yameelezwa leo na Shirika la Msalaba Mwekundu.
Maafisa wa serikali katika nchin za Bangladesh, India na Nepal wameitaja idadi ya watu walioaga dunia katika mafuriko hayo kuwa ni zaidi ya 750 tangu tarehe 10 mwezi huu, kufutia kunyesha mvua kubwa za msimu. Jagan Chapagain, Naibu Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu amesema kuwa hali ya mambo inazidi kuwa mbaya na kwamba karibu theluthi moja ya Nepal imeathirika na mafuriko. Ameongeza kuwa theluthi moja ya Bangladesh nayo pia imefurika.
Mafuriko hayo yaliyozikumba nchi hizo tatu yamewaacha katika hali ngumu mamia ya raia huku njia za barabara zikiharibika pia. Vijiji vingi huko India, Nepal na Bangladesh vinafikiwa kwa kutumia usafiri wa boti huku upungufu wa chakula na maji safi pia ukiripotiwa katika vijiji hivyo.