Stratijia mpya ya kijeshi ya Marekani nchini Afghanistan
Hatimaye baada ya miezi kadhaa ya mizozano katika timu ya usalama wa taifa ya Marekani, siku ya Jumatatu iliyopita Rais wa nchi hiyo Donald Trump, alitangaza stratijia mpya ya vita ya Washington kuhusiana na Afghanistan sambamba na mpango wa kutuma askari zaidi nchini humo.
Inatazamiwa kuwa katika stratijia hiyo mpya, askari zaidi wa Marekani watapelekwa nchini Afghanistan ambapo Trump atatoa idhini ya kutumwa wengine askari elfu nne ndani ya taifa hilo. Askari hao wapya wa Marekani watajumuishwa na wenzao 8,400 walioko hivi sasa nchini Afghanistan pamoja wengine elfu tano wa Muungano wa Kijeshi wa NATO. Marekani inataraji kwamba, itaungwa mkono na waitifaki wake katika NATO katika kutekeleza stratijia yake mpya nchini Afghanistan.
Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alitangaza kuwa, chaguo la kijeshi ni sehemu ya stratijia mpya ambayo imewasilishwa mbele ya Rais Donald Trump na ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea jinsi wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa NATO watakavyotoa mashirikiano katika suala hilo. Mattis ambaye amekabidhiwa na Trump majukumu ya kupanga na kutekeleza stratijia hiyo mpya ya Marekani kuhusiana na Afghanistan, ana wadhifa pia wa kuainisha kiwango cha askari wanaotakiwa kutumwa nchini humo. Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani anadai kuwa, ufanikishaji wa vipengee vya stratijia hiyo unategemea misaada itakayotolewa na wanachama wengine wa NATO. Baada ya miaka 16 ya uwepo kijeshi wa Marekani na NATO nchini Afghanistan, si tu askari hao haujaweza kuimarisha hata kidogo hali ya usalama ya nchi hiyo, bali kinachoshuhudiwa ni kurejea tena kundi la Taleban katika maeneo tofauti ya Afghanistan sambamba na kujitokeza tawi la kundi hatari la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) nchini humo na kuzidi kupungua kiwango cha usalama nchini humo.
Serikali ya Donald Trump inadai kuwa, kwa sasa haina njia nyingine ya kukabiliana na hali hiyo isipokuwa kutekeleza stratijia yake mpya ya kijeshi. Pamoja na hayo Washington haipendelei kujitosa kwenye uwanja huo peke yake. Kwa sababu tunaweza kutabiri kuwa Washington itatumia nyenzo zote ilizonazo kuwalazimisha wanachama wengine wa NATO wajiunge kwenye mpambano mpya wa kijeshi nchini Afghanistan. Kwa mujibu wa James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, stratijia mpya ya Marekani nchini Afghanistan, itatekelezwa kupitia fremu ya kieneo na itajikita juu ya namna ya kuhitimisha vita nchini humo.
Japokuwa Mattis anadai kwamba stratijia hiyo haitajikita katika kuongeza idadi ya askari wa Magharibi nchini Afghanistan, lakini ushahidi uliopo unaonyesha kwamba, moja ya mihimili mikuu ya stratijia tajwa ni kujiimarisha na kujizatiti zaidi kijeshi kwa kutuma askari zaidi wa Marekani na NATO katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita.
Stratijia mpya ya kijeshi ya Marekani nchini humo inatangazwa katika hali ambayo weledi wa mambo wameitathmini hali ya mambo kuwa mbaya zaidi hususan katika uga wa kiusalama nchini Afghanistan hasa baada ya kushadidi mashambulizi ya wanachama wa makundi ya Taleban na Daesh (ISIS).
Uingiliaji kijeshi wa Marekani ndani ya taifa hilo ulioanza tangu mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, haukuwa na faida nyingine ghairi ya mauaji ya raia, kuongezeka machafuko katika maeneo tofauti ya nchi, kuimarishwa zaidi uwezo wa kundi la Taleban, kutangazwa uwepo wa tawi la Daesh, ongezeko kubwa la uzalishaji wa mihadarati na kushtadi harakati za makundi ya kufurutu ada katika nchi nyingine za jirani hususan mataifa ya Asia ya Kati. Kwa mujibu wa Dakta Muhammad Akbar, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan, pamoja na Marekani kutumia kisingizio cha mashambulizi ya Septemba 11 kwa ajili ya kufikia malengo yake maalumu kupitia kuivamia Afghanistan, hadi sasa imeshindwa kufikia malengo hayo katika eneo. Ukweli ni kwamba kuongeza idadi zaidi ya askari wa Magharibi nchini Afghanistan, hakuwezi kusaidia kupatikana uthabiti na usalama katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Kama alivyosema Barnett Rubin, mchambuzi wa masuala ya Afghanistan wa nchini Marekani kwamba, Afghanistan haitashuhudia amani na uthabiti kwa uwepo wa kudumu wa majeshi ya Marekani nchini humo.