Velayati: Waislamu wana nafasi muhimu katika ustaarabu wa mwanadamu
(last modified Thu, 24 Aug 2017 02:37:31 GMT )
Aug 24, 2017 02:37 UTC
  • Velayati: Waislamu wana nafasi muhimu katika ustaarabu wa mwanadamu

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad nchini Iran amesema Waislamu wana nafasi muhimu katika ustaarabu wa mwanadamu na waliweka msingi katika sayansi nyingi zikiwemo za tiba, nujumu na fizikia.

Dkt. Ali Akbar Velayati aliyasema hayo jana Jumatano katika mji wa Mashhad Kaskazini Mashariki mwa Iran katika sherehe za kufunga kikao cha "Warsha za Kitaalamu za Jumuiya ya Kimataifa  ya Wahadhiri Waislamu katika Vyuo Vikuu."

Velayati ambaye pia ni mwanachama wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu Iran amesema, Waislamu wa awali waliongoza katika uvumbuzi wa vitu vingi na kuongeza kuwa  kila unapotajwa ustaarabu wa mwanadamu, Uislamu ndio unaobeba bendera ya ustaarabu huo.

Dkt Velayati amesema Uislamu umejengeka katika msingi wa elimu na mantiki na kwa msingi huo imani ya Kiislamu ni moja ya sababu muhimu za kuibuka ustaarabu wa Kiislamu.

Dkt. Velayati ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kila sehemu ambayo Uislamu ulienea duniani, eneo hilo lilishuhudia ustawi wa utamaduni na ustaarabu.

Mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wahadhiri Waislamu katika Vyuo Vikuu

Amesema mfano wa wazi ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchi ambayo sasa pasina kuwepo utegemezi wa madola ajinabi imeweza kufikia mafanikio makubwa ya kielimu. Amesema iwapo nchi zingine za Kiislamu zitaiga uzoefu wa Iran basi ustaarabu wa Kiislamu utaweza kunawiri zaidi duniani.

Aidha amesema walimwengu wanapaswa kufahamishwa kuhusu historia ya ustaarabu wa Kiislamu na kwamba sawa na Wamagharibi, wao pia wana uwezo na ujuzi wa hali ya juu.

kikao cha "Warsha za Kitaalamu za Jumuiya ya Kimataifa  ya Wahadhiri Waislamu katika Vyuo Vikuu" kilianza tarehe 21 Agosti mjini Mashhad na kumalizika Jumatano.

Tags