Waislamu wa Canada wafanya sherehe ya kutangaza Uislamu halisi
Waislamu wa mkoa wa Alberta nchini Canada wamefanya sherehe iliyopewa jina la 'Siku ya Turathi za Kiislamu' kwa lengo la kuitangaza dini ya Uislamu kwa watu wasiokuwa Waislamu.
Kanali ya televisheni ya CBC News imeripoti kwamba Waislamu wa mkoa huo, wamewataka wakazi wote wa mji wa Calgary kuhudhuria sherehe hizo ili kuufahamu Uislamu halisi kinyume na taswira ghalati inayotolewa na makundi ya kigaidi kuhusu dini hiyo ya Mwenyezi Mungu. Kufuatia mwaliko huo, mamia ya wakazi wa mji wa Calgary wamekusanyika kwa wingi katika bustani ya Olympic Plaza na kuanza kujifunza historia ya Uislamu kupitia ratiba mbalimbali zilizowasilishwa katika sherehe hizo.
Msimu wa joto mwaka huu mji wa Calgary pia ulishuhudia maandamano kadhaa ya kupinga dini ya Uislamu, hata hivyo Imran Muhyid-Din, mkuu wa ofisi ya Kiislamu Amerika ya Kaskazini yenye makao yake mjini Calgary amesema kuwa, kufanyika sherehe za 'Siku ya Turathi ya Kiislamu' ni fursa muhimu kwa ajili ya kuinua mahusiano mazuri kati ya jamii ya wakazi wa mji huo. Katika sherehe hizo, David Manson Eggen Waziri wa Elimu wa Canada amesema kuwa, wakazi wa mji wa Calgary wamekusanyika pamoja ili kushuhudia tamaduni za Kiislamu na kuboresha mahusiano ya pande mbili. Sherehe hizo zilifanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Jumamosi na Jumapili ambapo zilihudhuriwa na watu wengi.
Licha ya kuwepo propaganda na kampeni ya kueneza chuki na ubaguzi dhidi ya dini ya Kiislamu hususan katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Waislamu wa Canada wameweza kuitisha sherehe hizo za dini ya Uislamu ambapo zimepokelewa kwa kiwango kikubwa.