Waislamu Indonesia waandamana kuwatetea wenzao wa Rohingya
Waislamu nchini Indonesia wamejitokeza kwa wingi mabarabarani kushiriki maandamano ya kulaani mauaji na jinai wanazofanyiwa Waislamu wenzao wa kabila la Rohingya huko Myanmar.
Katika maandamano hayo ya jana Jumamosi, waandamanaji hao waliokuwa wamekusanyika nje ya ubalozi wa Myanmar mjini Jakarta walisikika wakitoa nara za kulaani jinai dhidi ya Warohingya.
Baadhi yao walisikika wakisema "Waokoe Waislamu wa Rohingya" huku wengine wakishinikiza kutimuliwa balozi wa Myanmar mjini Jakarta.
Kadhalika waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango na maberamu yaliyokuwa na ujumbe wa kumkashifu kiongozi wa chama cha 'Umoja wa Kitaifa kwa ajili ya Demokrasia' nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi. Baadhi ya mabango hayo yaliyokuwa na picha ya mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel yalibeba anwani inayosema "Mwanamke asiye na utu.''
Maandamano hayo yamefanyika licha ya polisi ya Indonesia kukabiliana na waadamanaji kwa shabaha ya kuyazima.
Takwimu ramsi zinaonyesha kuwa watu 400 wamepoteza maisha katika jimbo la Rakhine tokea Ijumaa iliyopita hadi sasa, baadhi yao wakiuliwa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada katika oparesheni dhidi ya Waislamu; huku makumi ya wengine wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wakipoteza maisha wakati wakivuka mto kukimbia mapigano katika jimbo la Rakhine.