Kushtadi hatua dhidi ya wahajiri, Ulaya Mashariki
Katika hatua ya kutekeleza siasa zake dhidi ya uhajiri, serikali ya Hungary imeutaka Umoja wa Ulaya kulipa nusu ya gharama za kuanzishwa mzingiro wa kimpaka wa nchi hiyo kwa lengo la kuwazuia wahajiri kuingia nchini humo.
Viktor Orbán, Waziri Mkuu wa Hungary wa mrengo wa kulia amedai kuwa, mzingiro huo si tu kwamba utasaidia kuikinga nchi yake na wimbi la uhajiri, bali utazikinga pia nchi nyingine za umoja huo kunako suala hilo. Tangu mwishoni mwa mwaka 2015 Hungary sambamba na kuweka vikwazo, vizuizi na kadhalika senyenge katika mpaka wake na Serbia na Croatia, ilizuia pia upenyaji wa wahajiri kuingia ardhi ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo mashirika ya haki za binaadamu yamekuwa yakitaka uzingatiaji wa dunia kuhusiana na hali mbaya na mienendo ya isiyokuwa ya kibinaadamu inayofanywa na baadhi ya serikali dhidi ya wahajiri na wakimbizi hususan katika nchi za Ulaya Mashariki wakati wanapojaribu kuvuka kuelekea upande wa Ulaya Magharibi.
Hata hivyo isisahaulike kuwa si Hungary peke yake ambayo inatekeleza miamala isiyo ya kibinaadamu dhidi ya wahajiri huko upande wa Ulaya Mashariki, bali hata jirani yake yaani Poland ambayo inaongozwa na serikali ya mrengo wa kulia, nayo imefuata siasa zile zile za Hungary kuhusiana na suala hilo. Ili kuzuia kuingia wakimbizi na wahajiri ambao kwa sasa wako nchini Ugiriki, baadhi ya nchi za Ulaya zimeamua kuweka vizuizi na mzingiro mpakani ikiwemo pia kuweka maafisa wa usalama na jeshi katika maeneo hayo ya mpakani kwa lengo la kuwazuia watu hao ambao walielekea barani humo kwa ajili ya kutafuta maisha bora. Kabla ya kuwekwa senyenge katika mpaka wa Hungary, karibu wahajiri laki nne walikuwa wamevuka nchi hiyo kuelekea Ulaya Magharibi. Mgogoro wa wahajiri ni changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya hivi sasa kwa kuzingatia ukubwa na utata wake na kadhalika misimamo ya kugongana ya nchi za umoja huo.
Ili kuainisha hatma ya wahajiri ambao wako barani humo, mwaka 2015 Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ilipasisha mpango wa kugawana wahajiri kati ya nchi wanachama. Pamoja na hayo nchi za Hungary, Jamhuri ya Czech, Slovakia, Romania na Poland ziliupigia kura ya hapana mpango huo, huku baadhi ya nchi zikiamua kutupilia mbali pendekezo hilo la Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EU) muda mfupi baadaye. Mbali na Hungary kupinga kwa maneno pendekezo hilo, ilichukua hatua za kivitendo kama vile kuanzisha mzingiro na kuweka vizuizi katika mpaka wake. Suala hilo limepelekea serikali ya Budapest na Warsaw kuwekewa vikwazo na kuchukuliwa hatua nyingine ya kisheria na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya.
Kwa mujibu wa Dimitris Auromopoulos, Kamishna wa Uhamiaji wa Umoja wa Ulaya, nchi za umoja huo ni lazima zitekeleze ahadi zao kuhusiana na suala hilo. Hata hivyo katika hali ambayo nchi hizo zinadai kuwapokea wahajiri kwa mujibu wa mafungu yaliyoainishwa na Kamisheni ya EU, zimeanza kuonyesha wasiwasi wao kwa kile kinachotajwa kuwa ni kutokea mabadiliko katika muundo wa kijamii na kiutamaduni wa nchini hizo kutokana na uwepo wa wahajiri. Oliver Angley mtaalamu wa masuala ya wahajiri anakiri jambo hilo kwa kusema: "Ulaya Mashariki kuna upinzani mkubwa juu ya suala zima la wahajiri." Mwisho wa kunukuu.
Licha ya kuongezeka mashinikizo makali ya Umoja wa Ulaya na hata kufikia kuziwekea vikwazo baadhi ya nchi wanachama zilizoonyesha upinzani wao, bado serikali za nchi hizo zinaendelea kushikilia msimamo wao wa kukataa kuwapokea wahajiri na wakimbizi. Inaonekana kuwa, tofauti na mpasuko juu ya suala la wahajiri bado litaendelea kushuhudiwa kiasi cha kuzifanya baadhi ya nchi kupendelea kujiondoa katika umoja huo. Msimamo wa serikali ya Hungary mbali na kuonyesha upinzani wake kivitendo, na kuamua kutaka msaada wa kifedha kwa ajili ya kuwazuia wahajiri wanaoingia nchini humo, unaonyesha ni kwa kiasi gani serikali ya Budapest isivyoheshimu sheria na maamuzi ya EU.