Dunia yaunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran, Marekani yatengwa zaidi
Kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na nchi za 5+1 kimefanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kwa lengo la kutathmini utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji-JCPOA.
Katika kikao hicho kilichofanyika chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Bi. Federica Mogherini, washiriki wote, isipokuwa Marekani waliyataja mapatano ya JCPOA kuwa mazuri huku wakipinga pendekezo la Washington la kuyaangalia upya.
Akizungumza na waandishi habari baada ya kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alisema, isipokuwa Marekani, wanachama wengine wote wa 5+1, yaani Uingereza, Ufaransa, Russia, China na Ujerumani, walisisitiza kuhusu kuzingatiwa kikamilifu mapatano ya JCPOA. Aidha walipinga pendekezo la Marekani la kufanya mazungumzo mapya kuhusu mapatano hayo ambayo wameyataja kuwa mafanikio ya kimataifa.
Kikao hicho cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA mjini New York kwa mara nyingine kilidhihirisha mtazamo wa pamoja wa nchi za Ulaya, China na Russia kuhusu umuhimu na ulazima wa kutetea mapatano hayo ya nyuklia ya Iran. Nchi zote katika kikao hicho pia zilikiri kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana kikamilifu na JCPOA. Lakini Marekani imechukua mkondo potovu wa kisiasa kuhusu mapatano hayo ya nyuklia ambayo yameidhinishwa pia kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Marekani sasa inayapinga mapatano hayo ambayo iliyasaini na inataka kufanyike mazungumzo mapya. Washiriki wa kikao hicho walijadili kuhusu namna Marekani inavyokiuka mapatano hayo ya JCPOA. Nchi hizo pamoja na Iran zimepinga vikali sera za Marekani za kutaka kuvuruga mapatano.
Ukweli ni kwamba mapatano ya JCPOA hayafungamani na nchi kadhaa tu bali ni mapatano ya kimataifa kwani yaliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa hivyo, kujiondoa katika mapatano hayo, kama inayvotaka kufanya Marekani, ni jambo linaloashiria kutowajibika nchi hiyo mbele ya ahadi zake za kimataifa. Pamoja na kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na nchi za 5+1 zimethibitisha kuwa Iran imefungamana na mapatano ya JCPOA, duru nchini Marekani zinadokeza kuwa Rais Trump tayari ameshachukua maamuzi ya mwisho kuhusu mapatano hayo lakini bado hajatangaza wazi msimamo wake. Baada ya hotuba ya kijinga ya Trump katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Iran na JCPOA, Nickey Halley, Balozi wa Marekani katika umoja huo amesema hotuba hiyo haimaanishi Washington inajiondoa katika JCPOA.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa Marekani inataka kufanya mazungumzo mapya kuhusu mapatano hayo ili kuondoa kile watawala wa Washington wanachodai ni nuksani katika JCPOA. Iwapo kama inavyotrajiwa pendekezo hilo la MarekanI litapingwa, kama alivyosema Rex Tillerson Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, nchi yake itachunguza kujiondoa katika JCPOA. Msimamo huu wa Marekani umepingwa na wanachama wenzake katika kundi la 5+1. Kuhusiana na hili Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya akizungumza mjini New York Jumatano alisema hakuna udharura wa kuangaliwa upya mapatano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran naye pia akizungumza na waandishi habari jana mjini New York kabla ya kurejea Tehran alisisitiza kuwa: "Hakuna mazungumzo mapya au marekebisho yanayoweza kufanyiwa mapatano ya JCPOA, na hivyo Wamarekani waondoe akilini fikra hiyo."
Kwa vyovyote vile, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa jibu linalofaa iwapo Marekani itatekeleza sera zake za uhasama na kuchukua hatua dhidi ya mapatano ya JCPOA. Kama alivyosisitiza rais wa Iran, kujiondoa Marekani katika JCPOA hakutaishinikiza Iran bali nchi hii itakuwa na nafasi nzuri zaidi duniani kuliko miaka ya nyuma na ni Markeani ndiyo itakayoshinikizwa na kutengwa na waliowengi duniani.